Breaking🔥

MKURUGENZI FRANONE AIPONGEZA SERIKALI, ATAKA UTAFITI ZAIDI KUINUA TANZANITE

FRANONE YATAKA UTAFITI ZAIDI KUINUA UZALISHAJI TANZANITE

Na Joseph Ngilisho | MERERANI

MKURUGENZI wa Kampuni ya Franone Mining Gems Ltd, Onesmo Mbise, amesema changamoto kubwa inayoikabili kampuni hiyo kwa sasa ni kushuka kwa uzalishaji wa madini ya Tanzanite, kutokana na maeneo ya awali yenye madini kumalizika na shughuli za uchimbaji kuhamia kwenye mikondo ya chini ya ardhi.


Mbise alisema hayo AGOSTI 24,2026 wakati akieleza changamoto mbele ya Waziri wa Madini ,Anthony Mavunde zinazoikabili kampuni hiyo katika shughuli za uchimbaji wa Tanzanite, akisisitiza umuhimu wa Serikali kuongeza nguvu katika utafiti ili kubaini maeneo mapya yenye madini na kuimarisha uzalishaji.

Alisema maeneo yaliyokuwa yakitumika katika hatua za awali za uchimbaji yameanza kumalizika, hali iliyosababisha shughuli za uchimbaji kuelekezwa katika mikondo ya chini ya ardhi ambayo inahitaji utafiti na utaalamu zaidi.

“Ukweli, changamoto kubwa hapa ni uzalishaji. Kwa kipindi hiki uzalishaji ni mgumu kwa sababu eneo lilikuwa na chimbo mwanzo na mikondo ya awali sasa imekwisha. Kilichobaki ni mikondo ya chini ambayo tunaendelea kuifuata,” alisema.

Alisema kampuni hiyo imepokea maelekezo ya Serikali ya kufanya utafiti zaidi katika eneo la Mererani, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kubaini maeneo mapya yenye Tanzanite na kurejesha uzalishaji katika kiwango kinachotarajiwa.

Mbise alisema tayari timu imeundwa chini ya uongozi wa Kamishna wa Madini, Dk Mwanga, kwa ajili ya kufanya utafiti huo, huku Franone ikiwa tayari kutoa utaalamu wake na kushirikiana na Serikali katika kutafuta suluhisho la changamoto hiyo.

“Tumezipokea maelekezo ya kufanya utafiti zaidi. Tayari kuna timu imeundwa inayoongozwa na Kamishna wa Madini, Dk Mwanga, na tutatoa utaalamu wetu na kuhakikisha tunashiriki pamoja ili tupate ufumbuzi na hali irudi kama kawaida,” alisema.

Alisema utafiti huo ukifanyika kwa kina unaweza kusaidia kubaini mikondo mipya ya madini na kutoa nafasi ya kuendeleza uchimbaji wa Tanzanite kwa muda mrefu, hatua ambayo pia itasaidia kuongeza uzalishaji na mapato yatokanayo na madini hayo.

Franone Mining inahusika na uchimbaji wa Tanzanite katika Kitalu C, Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post