Na Joseph Ngilisho|LONGIDO
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oberd Njipai, aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za Kamati kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2026 katika kikao cha Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Longido.Njipai alisema Kamati imebaini changamoto ya utoro shuleni na kusisitiza kuwa suala hilo haliwezi kuachwa kwa walimu pekee, bali linahitaji ushirikiano wa viongozi wa serikali za vijiji, madiwani, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.
Alisema, Madiwani wanapaswa kuwa sehemu ya juhudi hizo kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na wataalamu wa elimu ili kuhakikisha taarifa za wanafunzi wanaotoroka au kuacha shule zinatolewa kwa wakati na hatua stahiki zinachukuliwa.
“Hata sisi Waheshimiwa Madiwani tuwe sehemu ya kudhibiti utoro. Tuwaalike wataalamu, wakiwemo wakuu wa shule na walimu, katika kata zetu ili tushirikiane kuhakikisha tunatoa taarifa kwa wakati kuhusu watoto wanaoacha shule,” alisema Njipai.
Aidha, Kamati imeitaka Serikali ya Wilaya kusimamia mikakati ya kubaini na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaowapa mimba wanafunzi na kusababisha kukatisha masomo yao.
Katika hatua nyingine, Kamati imependekeza Serikali, jamii na wadau kushirikiana katika ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu ya shule ili kukabiliana na upungufu wa madarasa, mabweni, nyumba za walimu, mabwalo, vyoo na ofisi.
Njipai alisema madiwani wanapaswa kushirikiana na wenyeviti wa vijiji pamoja na watendaji kuanzisha miradi hiyo kwa kuwahamasisha wananchi kushiriki, huku Serikali ikisaidia kukamilisha pale itakapopatikana fedha.
Kamati pia imependekeza viongozi wa vijiji kushirikiana na shule kutumia walimu wa kujitolea walio karibu na maeneo hayo, hususan vijana waliomaliza masomo na kusubiri ajira, ili kusaidia kukabiliana na upungufu wa walimu.
Kamati imeitaka Halmashauri kutoa kipaumbele kwa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa kupitia asilimia 20 ya mapato ya ndani ambayo haikupata fedha katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa mujibu wa Njipai, miradi hiyo ina thamani ya jumla ya Sh milioni 150 na inahusisha ukamilishaji wa nyumba za watumishi, madarasa pamoja na ununuzi wa samani za shule katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Longido.
Kamati pia imependekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kutenga fedha kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya ukarabati wa bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Matale lililokumbwa na moto.
Njipai alisema suala hilo linapaswa kupewa kipaumbele kutokana na changamoto inayowakabili wanafunzi baada ya bweni hilo kuungua.
Aidha, Kamati imeitaka Halmashauri kushirikiana na TANESCO kutafuta suluhisho la changamoto ya umeme katika Zahanati ya Ndare ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa ufanisi.
Kamati imewataka viongozi wa elimu kuhakikisha walimu wakuu wanafuata taratibu za utoaji wa adhabu kwa wanafunzi kwa mujibu wa miongozo na waraka wa elimu unaohusika.
Njipai alisema Kamati imebaini kuwa adhabu kali shuleni, ikiwemo viboko, zinaweza kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia baadhi ya wanafunzi kuogopa au kukataa kwenda shule.
“Kamati imeelekeza itumike taratibu iliyowekwa katika Waraka wa Elimu ili kuhakikisha adhabu zinatolewa kwa utaratibu na na mtu anayestahili, ambaye ni mkuu wa shule,” alisema.
Kamati pia imependekeza kuimarishwa kwa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa wa saratani, upatikanaji wa chanjo na matibabu, pamoja na kuhakikisha vituo vya afya vilivyokamilika vinatoa huduma kikamilifu na watumishi waliopangiwa vituo hivyo wanapatikana kwa wakati.
Afisa elimu wa Halmashauri hiyo, alisema takwimu za wiki iliyopita zinaonesha kuwa wanafunzi zaidi ya 50 hawapo mashuleni kutokana na utoro.
Mwisho.




Post a Comment