DIWANI MREMA AMLILIA LUKUMAY KERO ZA MAJI, UMEME MANYIRE
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
DIWANI wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, amemuomba Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumay, kusaidia kutatua changamoto za maji, umeme na barabara zinazowakabili wananchi wa kata hiyo, akisema huduma hizo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii.
Mrema alitoa ombi hilo katika Kijiji cha Mlangarini wakati wa ziara ya Dkt Lukumay ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Manyire, mradi unaogharimu Sh milioni 584.
Akizungumza katika ziara hiyo Agosti 9,2026, Mrema alisema changamoto ya maji ni miongoni mwa kero kubwa kwa wananchi, hasa wakati wa kipindi cha ukame ambapo upatikanaji wa maji hupungua na wakati mwingine kusababisha migogoro miongoni mwa wananchi.
Alisema maeneo ya Olmesera, Marurui na Makao Mapya bado yanakabiliwa na uhaba wa maji, huku baadhi ya vitongoji vikiwa havijaunganishwa kabisa na mtandao wa maji.
“Tunapoelekea kwenye miezi ya ukame, tunakuwa na upungufu mkubwa wa maji ambao wakati mwingine hupelekea migogoro na hata mapigano. Tunakuomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane ili kuweka mtandao mzuri zaidi wa maji,” alisema Mrema.
Alisema endapo mamlaka zinazohusika zitaunganisha nguvu na kupanua mtandao wa maji, maeneo mengi ambayo kwa sasa hayapati huduma hiyo yataweza kuunganishwa na kupunguza kwa kiasi kikubwa kero hiyo.
Katika hatua nyingine, Mrema alieleza changamoto ya umeme, akisema baadhi ya vitongoji bado havijafikiwa na huduma hiyo licha ya kuwa ni hitaji muhimu katika maisha ya wananchi.
Alisema Kitongoji cha Olmesera kinahitaji takribani nguzo 180 ili kukamilisha usambazaji wa umeme katika kaya zilizopo eneo hilo, wakati Mungano kinahitaji nguzo 165.
Kwa upande wa eneo la Manyire, ambako ujenzi wa Shule ya Sekondari Manyire unaendelea, alisema linahitaji takribani nguzo 30 ili shule hiyo pamoja na maeneo jirani yaweze kupata huduma ya umeme.
“Kitongoji hiki ambacho tupo na kinajengwa sekondari hii ya kisasa hakina umeme. Umeme umezunguka sehemu nyingine, lakini hapa hatuna. Tunahitaji nguzo kama 30,” alisema.
Mrema pia alimtaka Dkt Lukumay kuendeleza ushirikiano na wataalamu wa TANESCO na REA ili kupata suluhisho la changamoto hiyo, akisema utekelezaji wa mahitaji hayo utaongeza kasi ya maendeleo ya wananchi.
“Tunazo kero nyingi, lakini kubwa ni barabara, maji na umeme. Hizi tunaziomba ziendelezwe, huku sisi tukiendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine katika kupunguza changamoto zilizopo,” alisema.
Ziara ya Dkt Lukumay katika Kijiji cha Mlangarini ililenga pia kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Manyire, unaotekelezwa kwa thamani ya Sh milioni 584, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza miundombinu ya elimu katika eneo hilo.
ends.




Post a Comment