Breaking🔥

BRELA YAWATAKA WABUNIFU KUSAJILI UBUNIFU KUULINDA NA KUJIPATIA KIPATO

BRELA YAWATAKA WABUNIFU KUSAJILI UBUNIFU KUULINDA NA KUJIPATIA KIPATO

Na Hadija Bagasha | TANGA

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wabunifu, wavumbuzi na wataalamu mbalimbali nchini kusajili kazi na ubunifu wao ili kupata haki ya kisheria ya kuutumia, kuulinda dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa na kuugeuza kuwa fursa ya biashara, ajira na kipato.

Wakala huo pia umewataka wabunifu kuacha kuuchukulia ubunifu kama jambo la kawaida, badala yake watambue kuwa mawazo, teknolojia na kazi wanazozalisha zinaweza kuwa mali yenye thamani kubwa kiuchumi endapo zitasajiliwa na kulindwa ipasavyo.

Wito huo umetolewa na Afisa Usajili wa BRELA, Benedickson Willson, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga.



Willson alisema usajili wa ubunifu na kazi mbalimbali ni hatua muhimu inayomwezesha mbunifu kupata haki ya kipekee ya kutumia kazi yake na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu au taasisi inayoweza kuitumia bila ridhaa yake.

Alisema BRELA imeshiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wabunifu na wavumbuzi, kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kusajili kazi zao pamoja na kuwawezesha kupata huduma zinazohusiana na usajili wa biashara na mali miliki.

Kwa mujibu wa Willson, maonesho hayo yanayofanyika kuanzia Agosti 15 hadi 24, mwaka huu, ni fursa kwa wananchi kujifunza namna ubunifu unavyoweza kubadilishwa kutoka wazo na kuwa bidhaa au huduma yenye thamani na hatimaye kuchangia maendeleo ya mtu binafsi na Taifa.

“Watu wanachukulia ubunifu kwa mtazamo wa kawaida, lakini ubunifu ndiyo njia sahihi ya kuendeleza Taifa na kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,” alisema.

Alisema mbunifu anayesajili kazi yake hujengewa msingi wa kuitumia kibiashara na kulinda maslahi yake dhidi ya watu wanaoweza kuiga au kutumia ubunifu huo bila ruhusa.

Aidha, alisema usajili wa alama za biashara na huduma humwezesha mmiliki kulinda chapa yake dhidi ya bidhaa bandia au watu wanaoweza kutumia jina na alama yake bila idhini.

“Ukiwa umesajili alama yako ya biashara au huduma, unaweza kuzuia bidhaa bandia kutumia chapa yako bila kibali. Hii inakupa ulinzi wa kisheria na thamani ya kiuchumi ya chapa yako,” alisema.

Willson alisema ubunifu uliosajiliwa na kulindwa ipasavyo unaweza kuwa chanzo cha biashara, ajira na kipato kwa mmiliki, kwani unaweza kutumika katika shughuli za kibiashara, kuingia katika mikataba na taasisi nyingine au kuhamisha haki ya matumizi kwa makubaliano rasmi.

Alisema hatua hiyo inawawezesha wabunifu kunufaika moja kwa moja na mawazo na kazi zao badala ya kuona watu wengine wakitumia ubunifu huo na kujipatia manufaa bila wao kunufaika.

Akizungumzia ubunifu unaohusisha teknolojia, Willson alisema eneo hilo lina fursa kubwa zaidi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya teknolojia zinazotatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Alitaja baadhi ya ubunifu huo kuwa ni teknolojia zinazotumia akili bandia katika kurahisisha kazi zinazohitaji uwepo wa binadamu pamoja na vifaa vinavyoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu wa kuona na changamoto nyingine.

“Teknolojia mpya inayotatua changamoto fulani katika jamii inakuwa mali yenye thamani. Mbunifu anaweza kuitumia kibiashara au kuingia makubaliano na wadau mbalimbali kutokana na teknolojia hiyo,” alisema.

Alisema vijana wana nafasi kubwa ya kutumia ubunifu kama daraja la kujiajiri na kujenga vyanzo vya kipato, lakini akasisitiza kuwa mafanikio hayo yanaweza kupatikana kwa urahisi zaidi iwapo watachukua hatua za mapema kusajili na kulinda kazi zao.

Willson aliwataka wabunifu kuwa makini na matumizi yasiyoidhinishwa ya kazi zao, akisema kutosajili ubunifu kunaweza kuwaweka katika mazingira ya kupoteza haki na manufaa ya kiuchumi yanayotokana na kazi walizozalisha.

Alisema BRELA itaendelea kutumia maonesho, mikutano na majukwaa mbalimbali nchini kuwafikia wabunifu, wavumbuzi na wataalamu ili kuwapatia elimu kuhusu taratibu za usajili na umuhimu wa kulinda mali miliki.

“Tunawakaribisha wabunifu, wavumbuzi na wataalamu wenye ubunifu wa aina mbalimbali kuja kupata huduma na elimu hapa. Lengo ni kuhakikisha ubunifu wao unatambuliwa, unalindwa na hatimaye unakuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa,” alisema.

Alisema ushiriki wa BRELA katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ubunifu unavyoweza kubadilishwa kuwa fursa ya kiuchumi na kuchangia ujenzi wa uchumi wa Taifa.

Kwa hatua hiyo, alisema wabunifu wanapaswa kutambua kuwa mawazo, teknolojia na kazi wanazobuni si tu suluhisho la changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa, bali pia ni mali inayoweza kuwa na thamani kubwa kiuchumi iwapo itasajiliwa, kulindwa na kutumiwa kwa tija.

MWISHO

Post a Comment

أحدث أقدم