Breaking🔥

AJALI YA HELIKOPTA KENYA YAUA JASUSI WA ECUADOR NA MKEWE

MKUU WA UJASUSI ECUADOR, MKEWE MIONGONI MWA WATU SABA WALIOFARIKI KWA AJALI YA HELIKOPTA KENYA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKURUGENZI Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini Ecuador, Michele Sensi Contugi, pamoja na mkewe, ni miongoni mwa watu saba waliofariki dunia baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la Mlima Ololokwe, Kaunti ya Samburu nchini Kenya.

Ajali hiyo, iliyotokea Agosti 19, 2026, imeibua wasiwasi katika duru za kimataifa kutokana na hadhi ya mmoja wa waathirika, huku kukiwa na maswali iwapo ilikuwa ajali ya kawaida au huenda kulikuwa na tukio lililopangwa dhidi ya kiongozi huyo wa ujasusi.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa mamlaka za Kenya au Ecuador unaoonyesha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na kitendo cha kigaidi au hujuma.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya (KCAA) imethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, ikisema helikopta aina ya Eurocopter EC130 B4, yenye usajili 5Y-GYM, ilikuwa imetoka Loisaba kuelekea Ewasonyiro kabla ya kuanguka majira ya saa 3:13 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki.

Ripoti za awali zinaeleza kuwa helikopta hiyo, iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Lady Lorry, ilikuwa imesafiri kutoka Soyian-Laikipia kuelekea Loisaba Conservancy kabla ya kupata ajali katika eneo la Mlima Ololokwe.

Mbali na kiongozi huyo wa Usalama wa Taifa wa Ecuador na mkewe, Wamarekani watano pia wamepoteza maisha katika ajali hiyo.

Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umethibitisha vifo vya raia wake watano, huku Telemundo ikiripoti kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha ni kiongozi wake, Jose Suarez.

Tukio hilo limezua taharuki kubwa katika eneo hilo, huku Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Samburu, David Nkoroi, akisema moshi mzito ulionekana ukitanda eneo la ajali muda mfupi baada ya helikopta hiyo kuanguka.

Nkoroi aliyeeleza kuwa vikosi vya uokoaji vilifika eneo la tukio kwa haraka, alisema mashuhuda waliripoti kuona moshi mweusi na moto mkubwa ukitoka katika eneo ambako helikopta hiyo ilianguka.

Taarifa hizo zilisababisha wakazi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama na kuchochea hatua za dharura, huku timu za uokoaji na wahudumu wa afya zikielekea eneo la tukio.

Mamlaka za Kenya zinaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo, huku taarifa zaidi zikitarajiwa kutolewa baada ya uchunguzi wa wataalamu wa usalama wa anga kukamilika.

Kifo cha Sensi Contugi kimeongeza uzito wa tukio hilo kimataifa, kutokana na nafasi yake nyeti katika usalama wa taifa wa Ecuador na mazingira ambayo alikuwa nchini Kenya.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post