PROFESA SAID MOHAMED AIBUKA RAIS MPYA WA AEAA, ASISITIZA NCHI ZA AFRIKA KUIMARISHA MIFUMO YA ELIMU
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
RAIS mpya wa Chama cha Tathmini ya Elimu Afrika (AEAA), Profesa Said Mohamed, kutoka Tanzania, ameahidi kuimarisha mifumo ya tathmini ya elimu barani Afrika huku akisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutumia fursa ya teknolojia, ikiwemo akili bandia (AI), kuboresha elimu na maandalizi ya vijana kwa mustakabali wa dunia.
Profesa Said, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), amechaguliwa kuongoza AEAA kwa kipindi cha mwaka 2026/2027, akirithi nafasi hiyo kutoka kwa Dkt Ashetu Kedege, katika kile kinachoelezwa kuwa mwanzo wa awamu mpya ya uongozi wa chama hicho.
Akizungumza leo Agosti 202026 baada ya kukabidhiwa rasmi uongozi huo katika Mkutano wa 42 wa AEAA uliofanyika Arusha, Profesa Said alisema amepokea dhamana hiyo kwa fahari na ari, akiahidi kutumia uzoefu na uwezo wake kuimarisha nafasi ya AEAA katika kujenga mifumo bora ya tathmini barani Afrika.
“Nimekubali kuwa Rais wa AEAA kwa mwaka 2026/2027 kwa fahari na ari. Nitatoa juhudi zangu zote, muda wangu na uwezo wangu kutekeleza wajibu na majukumu ya nafasi hii,” alisema.
Alisema uongozi wake utajikita katika kulinda, kuimarisha na kuendeleza AEAA, kusukuma maendeleo kwa pamoja na kujenga mifumo ya tathmini inayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Profesa Said alisema kuibuka kwa AI kunailazimisha Afrika kufikiria upya namna elimu na tathmini zinavyotolewa, akisisitiza kuwa bara hilo haliwezi kuendelea kutumia mifumo iliyoundwa kwa mazingira ya zamani wakati teknolojia inabadilisha kwa kasi namna watu wanavyojifunza na kufanya kazi.
“Miaka 20 iliyopita, AI ilikuwa maono ya siku zijazo, lakini leo siku zijazo tayari zinaanza kuonekana kwa kasi kubwa,” alisema.
Alisema AI inapaswa kutumiwa kama nyenzo ya kuboresha tathmini, si kuchukua nafasi ya wataalamu katika kufanya maamuzi ya kitaalamu.
Kauli hiyo inaendana na maazimio ya mkutano huo yaliyosisitiza matumizi yenye uwajibikaji ya AI katika tathmini, huku yakitaka kuwepo kwa uwazi, uwajibikaji, haki, ushirikishwaji, ulinzi wa taarifa na uadilifu wa mitihani.
Mkutano huo ulifikia maazimio 11, yakiwemo kuandaa sera na viwango vya matumizi ya AI, kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika utafiti na ubunifu, kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali na kujenga uwezo wa wataalamu wa tathmini.
Aidha, vyombo vya tathmini vilihimizwa kuimarisha usalama wa mitihani ya kidijitali, ulinzi wa taarifa na uthibitishaji wa utambulisho wa watahiniwa, huku vikiepuka kutegemea kupita kiasi teknolojia za kubaini udanganyifu baada ya kutokea.
Profesa Said alisema rasilimali kubwa zaidi ya Afrika si madini, ardhi wala maliasili nyingine, bali ni watu wake, ambao wakipata elimu bora wanaweza kubadilisha mustakabali wa bara hilo.
Akirejea sehemu ya wimbo wa Taifa wa Tanzania unaosema “Mungu ibariki Afrika, tubariki watoto wa Afrika,” alisema baraka kubwa zaidi kwa watoto wa Afrika ni kupata elimu bora na fursa sawa.
Alisema AEAA ina wajibu wa kuhakikisha kila mtoto anatambuliwa kama rasilimali muhimu anayestahili kupata elimu bora na mfumo wa tathmini wenye haki.
Akisisitiza umuhimu wa mshikamano, Profesa Said alisema mafanikio ya AEAA hayawezi kupatikana kwa mtu mmoja, bali yanahitaji ushirikiano, kuheshimiana na kuaminiana miongoni mwa wanachama.
“Hatuko timu kwa sababu tu tuko pamoja; sisi ni timu kwa sababu tunaaminiana, tunaheshimiana na tunajali kila mmoja,” alisema.
Pia alisisitiza dhana ya uongozi wa kuhudumia wengine , akisema uongozi haupaswi kuonekana kama fursa ya kupata mamlaka au hadhi, bali ni dhamana ya kutumikia maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Katika hotuba yake, Profesa Said alimpongeza Dkt Ashetu Kedege kwa uongozi wake na mchango wake katika kuiimarisha AEAA.
Alisema Dkt Kedege ataendelea kuwa sehemu ya uongozi wa chama hicho kama Rais Mstaafu wa Mara Moja (Immediate Past President) na mjumbe wa Bodi kwa mujibu wa Katiba ya AEAA.
Profesa Said alisema chama hicho kitaendelea kunufaika na hekima, utaalamu, uzoefu na kujituma kwa Dkt Kedege, akimtakia afya njema na mafanikio katika miaka ijayo.
Kwa upande wake, Dkt Kedege alihitimisha rasmi kipindi chake cha uongozi wakati wa kufungwa kwa Mkutano wa 42 wa AEAA, ambao pia ulipitisha tamko linalotaka serikali, taasisi za elimu, sekta binafsi, vituo vya utafiti na washirika wa maendeleo kushirikiana kujenga mifumo ya tathmini iliyo imara, bunifu, shirikishi, salama na inayokidhi mahitaji ya zama za kidijitali.
Mbali na ajenda ya AI, mkutano huo uliweka msisitizo katika tathmini inayozingatia umahiri, ujifunzaji endelevu, matumizi ya data, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (TVET), pamoja na ushirikiano kati ya taasisi za elimu na viwanda.
Mkutano pia ulitaka matumizi ya tathmini zinazotegemea mazingira halisi na utendaji ili kupima uwezo wa wanafunzi katika kufikiri kwa kina, kutatua matatizo, kufanya maamuzi na kutumia maarifa katika mazingira halisi.
AEAA pia ilisisitiza umuhimu wa mifumo ya mrejesho wa kidijitali inayoweza kutoa taarifa kwa wakati ili kusaidia kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na utendaji wa taasisi za elimu.
Uchaguzi wa Profesa Said unaipa Tanzania nafasi muhimu katika kuongoza mjadala wa tathmini ya elimu barani Afrika wakati ambapo nchi nyingi zinakabiliwa na mapinduzi makubwa ya kiteknolojia, kuongezeka kwa matumizi ya AI na hitaji la kubadilisha mifumo ya elimu ili iendane na mahitaji ya kizazi kijacho.
Akihitimisha hotuba yake, Profesa Said aliwataka wataalamu wa elimu barani Afrika kutosubiri mabadiliko yawafikie, bali wayatangulie kwa ubunifu, ushirikiano na uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya elimu na tathmini.
“Tusitembee na mustakabali; tukimbie kuelekea mustakabali, kwa sababu mustakabali mzuri uko mbele yetu,” alisema.
ENDS..







Post a Comment