MSUMI ATUNUKIWA TUZO KWA MCHANGO KWA WATU WENYE UALBINO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC), Seleman Msumi, ametunukiwa tuzo kwa kutambua mchango wake wa hali na mali katika kusaidia watu wenye ualbino na kuiwezesha Taasisi ya Empower Albinism Tanzania kukua na kujitegemea.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Empower Albinism Tanzania, Japhet Tasha Lukumay, ambaye alisema Msumi amekuwa mstari wa mbele kuiunga mkono taasisi hiyo tangu ilipoanzishwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo, Tasha alisema Msumi amekuwa akitoa fedha pamoja na misaada mbalimbali, hatua ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuiwezesha taasisi hiyo kukua na kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwasaidia watu wenye ualbino.
Alisema msaada wa Msumi umekuwa na thamani kubwa katika safari ya taasisi hiyo na bila mchango wake huenda Empower Albinism Tanzania isingefikia hatua iliyonayo kwa sasa.
“Tunamshukuru sana Mkurugenzi Mtendaji kwa moyo wake wa kutusaidia tangu tulipoanza. Mchango wake wa hali na mali umetuwezesha kufikia hatua hii na kusimama kama taasisi,” alisema Tasha.
Alisema tuzo hiyo ni sehemu ya kutambua mchango wa watu ambao wamekuwa wakisimama pamoja na taasisi hiyo katika kuhakikisha watu wenye ualbino wanapata fursa na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Msumi alisema amekuwa akiona umuhimu wa kusaidia jamii ya watu wenye ualbino kwa kuwa wana haki ya kujitegemea, kuendesha shughuli zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Alisema jukumu la kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu si jambo aliloanza akiwa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha pekee, bali ni sehemu ya misingi ambayo amekuwa nayo katika maeneo mbalimbali aliyowahi kufanya kazi.
Msumi alisema bado ni mwanachama katika vituo mbalimbali vinavyowahudumia watu wenye mahitaji maalumu, wakiwemo watu wenye ualbino, akisisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kuwaunga mkono.
Aidha, Msumi aliishukuru Empower Albinism Tanzania kwa kutambua mchango wake, huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kuiunga mkono taasisi hiyo na watu wenye ualbino.
Alisema pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa, bado watu wenye ualbino wanakabiliwa na mahitaji muhimu, ikiwemo mafuta ya kujikinga na miale ya jua, kofia na mahitaji mengine yanayosaidia kulinda afya zao.
Alisema ushirikiano kati ya jamii, Serikali na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha watu wenye ualbino wanapata fursa sawa, wanajiamini na wanaweza kujitegemea katika maisha yao.

Post a Comment