WATU SITA WALIOLIPUA BOMU KANISA LA MT YOSEPH MFANYAKAZI OLASITI NA KUHUKUMIWA KUNYONGWA NA KUKATA RUFAA, MAHAKAMA YA RUFANI YATHIBITISHA HUKUMU YA KIFO

WATU SITA WA BOMU OLASITI WAPOTEZA MATUMAINI YA RUFANI

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

WATU sita waliokuwa wakisaka nafuu kupitia rufaa baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa makosa ya mauaji na ugaidi kufuatia shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti jijini Arusha, wamepoteza matumaini hayo baada ya Mahakama ya Rufani kuthibitisha hukumu dhidi yao.

Uamuzi huo umehitimisha safari ya miaka 13 ya kutafuta haki tangu shambulio hilo la kigaidi lililotokea Mei 5, 2013 na kusababisha vifo vya waumini watatu huku zaidi ya 50 wakijeruhiwa.

Mahakama ya Rufani imebainisha kuwa Mahakama Kuu haikukosea ilipowatia hatiani Abashari Omary, Yusuph Hutta, Ramadhani Waziri, Abdul Juma, Kassim Ramadhan na Japhari Lema kwa makosa ya mauaji, kutenda vitendo vya kigaidi na matumizi ya mali kwa kutenda vitendo vya kigaidi.

Katika hukumu iliyotolewa Jumatatu, Julai 27, 2026 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao, jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao ni Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Lameck Mlacha, lilisema ushahidi uliowasilishwa ulithibitisha makosa hayo bila kuacha shaka yoyote ya msingi.

Majaji hao walisema hakuna sababu ya kuingilia hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu katika kesi ya jinai namba 32 ya mwaka 2023 iliyotolewa na Jaji John Nkwabi Desemba 12, 2023.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani imefuta hatia ya kosa la kula njama ya kutenda vitendo vya kigaidi, ikieleza kuwa kisheria kosa hilo haliwezi kusimama pale ambapo kosa la ugaidi lililokusudiwa tayari limethibitika na kutekelezwa.

“Katika mambo yote yaliyobaki, rufaa inakataliwa na hukumu za mauaji, kutenda vitendo vya kigaidi na matumizi ya mali kwa kutenda vitendo vya kigaidi zinathibitishwa,” imeeleza hukumu hiyo.

Rufaa hiyo ya jinai namba 93 ya mwaka 2024 ilikatwa na warufani hao dhidi ya Jamhuri, wakipinga hukumu na adhabu waliyopewa na Mahakama Kuu.

Bomu lililovunja shangwe Olasiti

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi, Mei 5, 2013 mamia ya waumini walikuwa wamekusanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti jijini Arusha kwa ajili ya uzinduzi wa parokia hiyo mpya.

Katika hafla hiyo, Balozi wa Papa nchini Tanzania wakati huo, Askofu Francisco Padilla, pamoja na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Josephat Lebulu, walinusurika baada ya bomu kurushwa katikati ya umati wakati wa kukata utepe wa uzinduzi.

Tukio hilo lililokuwa la shangwe lilibadilika ghafla kuwa majonzi baada ya mlipuko huo kuua waumini watatu na kujeruhi zaidi ya 50.

Baada ya tukio hilo, uchunguzi ulifanywa na watu 10 walikamatwa na kushtakiwa mwaka 2014. Mmoja kati yao alifariki kabla ya kuanza kwa kesi, huku wengine watatu waliachiwa huru wakati wa hukumu.

Katika kesi hiyo, washitakiwa walikabiliwa na makosa ya kula njama ya kutenda vitendo vya ugaidi, kutenda vitendo vya ugaidi, mauaji na kutumia mali kuwezesha kutendeka kwa vitendo vya kigaidi.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa kabla ya shambulio hilo kulifanyika mkutano wa kupanga tukio nyumbani kwa mmoja wa washtakiwa, Ramadhani Waziri, huku taarifa kuhusu ratiba ya sherehe za kanisa zikidaiwa kutolewa na Japhari Lema.

Mashtaka yalitegemea ushahidi wa mashahidi, vielelezo vya uchunguzi, ushahidi wa kitabibu pamoja na maelezo ya onyo ya baadhi ya washtakiwa ambayo yalijadiliwa katika kesi ya msingi.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mahakama Kuu iliwatia hatiani washtakiwa hao kwa makosa ya mauaji, ugaidi, matumizi ya mali kwa kutenda vitendo vya ugaidi na kula njama ya kutenda ugaidi, na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa.

Wakiwa hawajaridhishwa na hukumu hiyo, walikata rufaa wakidai Mahakama Kuu ilikosea kisheria na kiutaratibu kwa kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi yao bila kuacha shaka yoyote ya msingi.

Walidai pia kuwa Mahakama haikufanya tathmini ya kina ya ushahidi wa pande zote, ilitegemea vielelezo visivyokubalika kisheria na ilitumia maelezo ya ungamo yaliyokataliwa.

Katika sababu nyingine ya rufaa, walidai Mahakama ilikosea kuwatia hatiani kwa wakati mmoja kwa kosa la kula njama ya kutenda vitendo vya ugaidi na kutenda vitendo hivyo, wakisema makosa hayo hayawezi kusimama pamoja pale kosa la msingi linapokuwa limethibitika.

Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, warufani hao waliwakilishwa na mawakili tisa huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wa Serikali waandamizi watano.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post