MAHAKAMA KUU YA TANZANIA YAIFUTA KESI YA UCHAGUZI KIGOMA MJINI, USHINDI WA BABA LEVO WABAKI SALAMA
Na Joseph Ngilisho|Arushadigital
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, imeifuta kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Jimbo la Kigoma Mjini, hivyo kuthibitisha kuendelea kusimama kwa ushindi wa Mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Levocatus Chipando maarufu Baba Levo.
Uamuzi huo ulitolewa leo Alhamisi, Julai 16, 2026 na Jaji Victoria Nongwa, aliyesema walalamikaji walishindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha unaoweza kuijengea Mahakama msingi wa kuwataka wajibu maombi kuanza kujitetea.
Jaji Nongwa alisema baada ya kuchambua ushahidi wote uliowasilishwa mbele ya Mahakama, ilibainika kuwa haukufikia kiwango kinachotakiwa kisheria kuendelea na hatua inayofuata ya usikilizwaji wa shauri, hivyo akaamuru kesi hiyo ifutwe.
Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 ilitokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ambapo Baba Levo alitangazwa mshindi wa kiti cha Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini.
Shauri hilo lilifunguliwa na wananchi wanne waliodai kuwa ni wapiga kura wa jimbo hilo ambao ni Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo Kombolela na Lumu Mwitu, wakidai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi na kuiomba Mahakama ibatilishe matokeo pamoja na ushindi wa Baba Levo.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia ushahidi uliowasilishwa, Mahakama ilihitimisha kuwa madai hayo hayakuthibitishwa kwa kiwango kinachohitajika kisheria.
Uamuzi huo unaweka mwisho wa shauri hilo na kuacha ushindi wa Levocatus Chipando (Baba Levo) ukiendelea kuwa halali, huku akiendelea kutekeleza majukumu yake kama Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini.

إرسال تعليق