LUKUMAY AMTAKA MKURUGENZI WA HALMASHAURI KUSIMAMIA MIRADI, AONYA DHIDI YA UPOTEVU WA FEDHA ZA UMMA
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha (Arusha Dc) pamoja na timu ya wataalamu kutoka idara mbalimbali kuhakikisha wanashuka mara kwa mara vijijini kutembelea, kukagua na kusimamia miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo miradi ya Mfuko wa Jimbo, ili kuhakikisha ubora wa kazi unalingana na thamani ya fedha zilizotolewa na hivyo kuzuia upotevu wa fedha za umma zinazotokana na kodi za wananchi.
Mbunge Lukumay, amesema ni wakati wa wataalamu kutoka halmashauri kuondoka maofisini na kwenda vijijini kufuatilia utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kama ilivyokusudiwa
Amesema usimamizi wa karibu wa miradi ni silaha muhimu ya kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinawafikia wananchi kupitia miradi yenye ubora, badala ya kutumika vibaya kutokana na uzembe au ukosefu wa ufuatiliaji.
Alitoa kauli hiyo Julai 15,2026 katika Kijiji cha Losinoni Juu, Kata ya Oldonyowasi, wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo, sambamba na kusikiliza kero na maoni ya wananchi.
"Ninataka kuona wataalamu wanatoka ofisini na kwenda kwenye miradi. Kazi yao si kusubiri taarifa mezani pekee, bali kuhakikisha kila shilingi inayotolewa na Serikali inaleta thamani iliyokusudiwa. Hizi ni fedha za wananchi, hivyo lazima zilindwe," alisema Dkt. Lukumay.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupeleka fedha nyingi za maendeleo katika sekta mbalimbali, hivyo ni wajibu wa viongozi na wataalamu kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa ufanisi na miradi inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.
Katika ziara hiyo, Dkt. Lukumay alikagua mradi wa ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Namelock uliogharimu Shilingi milioni 12.6 kutoka Mfuko wa Jimbo, na kueleza kuridhishwa na ubora wa kazi pamoja na manufaa yake kwa wanafunzi na walimu.
Alisema uwekezaji huo umeboresha mazingira ya usafi shuleni, kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye vyoo na kuchangia kulinda afya zao.
Hata hivyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Namelock, Stephen Lazaro, alisema pamoja na mafanikio hayo, shule bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji msaada wa Serikali na wadau wa maendeleo.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni upungufu wa matundu mengine 14 ya vyoo, ukosefu wa mpango wa chakula cha mchana kwa wanafunzi, pamoja na uhaba wa vifaa vya TEHAMA ikiwemo mashine ya fotokopi na printer zinazohitajika katika shughuli za kila siku za shule.
Aidha, alisema shule hiyo pia inahitaji ujenzi wa nyumba za walimu ili kuwasaidia kuishi karibu na kituo cha kazi, hatua ambayo itaongeza morali wa kazi, kupunguza utoro wa walimu na kuboresha kiwango cha taaluma kwa wanafunzi.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwa wingi, Dkt. Lukumay aliwashukuru kwa kutoa maoni na kueleza changamoto zao kwa uwazi, akisema ushiriki wa wananchi unaisaidia Serikali kupanga miradi yenye kuakisi mahitaji halisi ya jamii.
Aliwahakikishia kuwa changamoto ambazo hazitapatiwa ufumbuzi katika ngazi ya halmashauri zitapelekwa katika wizara husika na bungeni ili zipatiwe ufumbuzi wa kudumu.
Kuhusu miundombinu ya barabara, mbunge huyo alisema barabara ya Jiji–Kisimiri yenye urefu wa kilomita 12 tayari imeidhinishiwa fedha na itajengwa kwa kiwango cha changarawe, hatua itakayorahisisha usafiri wa wananchi, usafirishaji wa mazao na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Katika sekta ya maji, alisema tayari ameiwasilisha bungeni changamoto ya maji yenye kiwango kikubwa cha madini ya fluoride katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, huku Serikali ikiendelea kutekeleza miradi ya maji.
Aliongeza kuwa Kijiji cha Msununi kimetengewa fedha kwa ajili ya kuchimbwa kisima kirefu kitakachoongeza upatikanaji wa maji safi na salama.
Katika tukio lililogusa hisia za wengi, Dkt. Lukumay alijikuta akitokwa na machozi baada ya kupokelewa na mamia ya wananchi waliomlaki kwa mila za Kimasai, wakimwombea mafanikio na kumkabidhi zawadi mbalimbali kama ishara ya kuthamini juhudi zake za kuwatumikia na kuwasemea bungeni.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Lazaro Laizer alisema wakazi wa Oldonyowasi wameanza kuona matunda ya uwakilishi wao na hawana cha kumlipa mbunge huyo zaidi ya kumwombea.
"Mheshimiwa Mbunge, sisi wananchi wa Oldonyowasi hatuna zawadi kubwa ya kukulipa zaidi ya kukuombea kwa Mungu. Tunakusikia ukitusemea bungeni na leo tunaona matokeo yake. Tunaomba uendelee na moyo huo wa kupigania maendeleo yetu," alisema Lazaro.
Akihitimisha ziara hiyo, Dkt. Lukumay alisema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kupeleka fedha za maendeleo katika Kata ya Oldonyowasi na maeneo mengine ya Arumeru Magharibi, huku akiwataka wananchi kushirikiana na viongozi katika kulinda, kusimamia na kuitunza miradi hiyo ili idumu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Ends..


إرسال تعليق