LUKUMAY AWAHAKIKISHIA WANANCHI WA OLDONYOWASI: BARABARA, MAJI NA MIRADI YA MAENDELEO ,APOKEWA KIFALME WANANCHI WAJILAUMU KUCHELEWA KUMCHAGUA,

 LUKUMAY AWAHAKIKISHIA WANANCHI WA OLDONYOWASI: BARABARA, MAJI NA MIRADI YA MAENDELEO KUTEKELEZWA

Na Joseph Ngilisho|ARUMERU

 

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amewahakikishia wananchi wa Kata ya Oldonyowasi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutatua changamoto zao kwa kutekeleza miradi ya maendeleo inayogusa maisha yao ya kila siku, ikiwemo barabara, maji, elimu na afya.

Dkt. Lukumay aliyasema hayo leo Julai 15,2026 wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Losinoni Juu, Kata ya Oldonyowasi, wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Mbunge, sambamba na kusikiliza kero za wananchi.

Katika ziara hiyo, mbunge huyo alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Namelock, uliogharimu Shilingi milioni 12.6 kutoka fedha za Mfuko wa Mbunge, akisema mradi huo umeboresha mazingira ya usafi na afya kwa wanafunzi na walimu.

Hata hivyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Namelock, Stephen Lazaro, alisema pamoja na mafanikio hayo, shule bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi wa haraka ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Alitaja mahitaji makubwa ya shule hiyo kuwa ni ujenzi wa matundu 14 ya vyoo ili kukidhi idadi ya wanafunzi waliopo, upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi, pamoja na vifaa muhimu vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo mashine ya fotokopi (Photocopy Machine) na mashine ya kuchapisha nyaraka (Printer).

Aidha, alisema shule hiyo inahitaji ujenzi wa nyumba za walimu ili kuwasaidia walimu kuishi karibu na kituo cha kazi, hatua ambayo itaongeza ari ya kazi na kuboresha kiwango cha elimu kinachotolewa kwa wanafunzi.

Akizungumza na wananchi, Dkt. Lukumay aliwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi na kueleza changamoto zao kwa uwazi, akisema ushiriki wao unaisaidia serikali kupanga na kutekeleza miradi inayojibu mahitaji halisi ya wananchi.

Pia aliwapongeza wataalamu wa halmashauri pamoja na taasisi mbalimbali kwa kujibu maswali ya wananchi, huku akisisitiza kuwa changamoto ambazo hazitapatiwa ufumbuzi katika ngazi ya halmashauri zitapelekwa bungeni na katika wizara husika.

Kuhusu miundombinu ya barabara, Dkt. Lukumay alisema barabara ya Jiji–Kisimiri yenye urefu wa kilomita 12 imeidhinishiwa fedha maalumu na itajengwa kwa kiwango cha changarawe ili kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika kata hiyo.

Katika sekta ya maji, alisema tayari ameiwasilisha bungeni changamoto ya maji yenye kiwango kikubwa cha madini ya fluoride, huku Serikali ikiahidi kukamilisha miradi ya maji inayoendelea. Aidha, alisema Kijiji cha Msununi kimetengewa fedha kwa ajili ya kuchimbwa kisima kirefu kitakachoongeza upatikanaji wa maji safi na salama.

Mbunge huyo aliwataka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, wakuu wa idara na wataalamu wa sekta mbalimbali kushuka mara kwa mara vijijini kusimamia miradi ya maendeleo na kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Katika hali isiyokuwa ta kawaida mbunge huyo alijikuta  akitokwa machozi baada kuona umati mkubwa wa wananchi wakimlaki kimila na kumwombea mafanikio huku wakimpa zawadi kedekede ,baada ya kuridhishwa na kasi ya utendaji wake wa kazi katika jimbo hilo ikiwemo kuwasemea bungeni changamoto zao.

"Mh. mbunge sisi wananchi wa kata ya Oldonyowasi hatuna cha kukulipa ila ni kukuombea kwa mungu maana tunakusikia sana ukitusemea bungeni,tunachoomba uendelee na moyo huo maana tulichelewa kukuchagua" alisema  Lazaro Laizer .

Akihitimisha, Dkt. Lukumay alisema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kupeleka fedha za maendeleo katika Kata ya Oldonyowasi na maeneo mengine ya Arumeru Magharibi, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi katika kulinda na kusimamia miradi hiyo ili ilete maendeleo endelevu kwa jamii.








**(Ends***

Post a Comment

أحدث أقدم