KAMBI YA AFYA YA MAKONDA YAVUNJA REKODI, WANANCHI 24,871 WAHUDUMIWA,WAGONJWA 258 WAHITAJI UPASUAJI MSAADA WAHITAJIKA

KAMBI YA AFYA YA MAKONDA YAVUNJA REKODI, WANANCHI 24,871 WAHUDUMIWA,AOMBA MSAADA WA UPASUAJI WAGONJWA 258

Na Joseph Ngilisho | Arusha

 

Zaidi ya wananchi 24,871 wamenufaika na huduma mbalimbali za matibabu kupitia kambi ya madaktari bingwa iliyofanyika kwa siku nane mfululizo jijini Arusha, huku wagonjwa 258 wakibainika kuhitaji upasuaji maalumu.

 Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, amewaomba wadau, wafanyabiashara na watu wenye mapenzi mema kujitokeza kusaidia kugharamia matibabu yao.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungwa kwa kambi hiyo, Makonda alisema lengo la kuandaa huduma hizo lilikuwa kuwasogezea wananchi matibabu ya kibingwa ambayo kwa kawaida hupatikana katika hospitali za rufaa kama KCMC, Benjamin Mkapa na Bugando, hivyo kupunguza gharama na usumbufu wa kusafiri kutafuta huduma.


Alisema wananchi wengi wamekuwa wakishindwa kupata matibabu ya kibingwa kutokana na changamoto za kifedha, hivyo wakaamua kuwaleta madaktari bingwa Arusha ili huduma zipatikane karibu na wananchi.

"Kulikuwa na watu waliokuwa wamekata tamaa kabisa ya kupata matibabu ya kibingwa. Leo wamepata huduma na kurejeshewa matumaini ya maisha," alisema Makonda.

Alisema jumla ya wataalamu 520, wakiwemo madaktari bingwa, madaktari wa kawaida, wauguzi na wataalamu wengine wa afya walifanya kazi mchana na usiku kuhakikisha wananchi wote waliojitokeza wanahudumiwa.

Aidha, alisema zaidi ya watu 200 walijitolea katika shughuli mbalimbali za uratibu, zikiwemo kupanga foleni, kugawa namba, kuelekeza wagonjwa na kuhakikisha mazingira yanakuwa salama na safi, hivyo kufanya jumla ya watu zaidi ya 720 kushiriki kufanikisha zoezi hilo.

Makonda alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana yameonyesha umuhimu wa kupeleka huduma za kibingwa karibu na wananchi, lakini bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha wagonjwa waliobainika kuhitaji upasuaji wanapata matibabu hayo.

"Kwa upande wetu kama ofisi ya Mbunge na timu yetu, tunatamani kuwaona wananchi hawa wote 258 wanafika hatua ya pili ya kufanyiwa upasuaji. Tunaomba Mungu atufungulie milango na kuwagusa watu wenye uwezo na wenye huruma washiriki kuokoa maisha ya ndugu zetu," alisema.

Alisema kila mgonjwa atakayefanyiwa upasuaji atakuwa ushuhuda wa nguvu ya mshikamano wa jamii katika kuokoa maisha ya Watanzania na kurejesha furaha kwa familia zao.

Mbunge huyo aliwashukuru madaktari, wauguzi, wataalamu wa afya na wote waliojitolea kwa kujitoa kwao katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

"Kwa niaba ya wananchi wa Arusha, ninawashukuru sana madaktari, wauguzi, wataalamu wa afya na wote waliojitolea. Wameleta matumaini mapya kwa watu waliokuwa wamekata tamaa ya kupata matibabu ya kibingwa," alisema.

Pia aliwashukuru wadau mbalimbali, taasisi, kampuni binafsi na Bohari ya Dawa (MSD) kwa kuchangia dawa, vifaa tiba, magari, ambulansi, chakula, maji na huduma nyingine zilizowezesha wagonjwa kuendelea kupata matibabu bila kukatishwa.

Makonda alisema hata pale baadhi ya dawa zilipoisha, kamati ya uratibu ilihakikisha zinanunuliwa kutoka maduka binafsi ili hakuna mgonjwa aliyeondoka bila kupata dawa alizoandikiwa.

Aliongeza kuwa kambi hiyo imebakiza kiasi kikubwa cha dawa na vifaa tiba ambavyo vitaendelea kutumika kuhudumia wananchi wenye mahitaji mbalimbali ya kiafya.

"Tulipata dawa nyingi kiasi kwamba zilibaki. Dawa hizo hazitapotea, zitaendelea kutumika kuwatibu wananchi wenye mahitaji mbalimbali ya kiafya. Huu ni ushahidi wa baraka ambazo Mungu ametujalia kupitia huduma hii," alisema.

Makonda pia alivipongeza vyombo vya habari kwa mchango mkubwa wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata huduma hizo, akisema matangazo yaliyotolewa na redio mbalimbali za Arusha, televisheni pamoja na vyombo vya habari vya kitaifa yamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya kambi hiyo.

Alisema ushirikiano huo umeongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa uchunguzi na matibabu ya mapema, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na sekta ya afya na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za kibingwa zinaendelea kuwafikia wananchi wa Arusha.





Ends


Post a Comment

أحدث أقدم