LISU AREJESHWA GEREZANI SHAURI LA KATIBA LIKIAHIRISHWA HADI SEPTEMBA 16

 SHAURI LA KATIBA LA LISSU LAAHIRISHWA HADI SEPTEMBA 16

By Arushadigital

Shauri la Kikatiba Na. 7300 la mwaka 2026, linalohusu madai ya kukiukwa kwa haki ya faragha ya mawasiliano kati ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, na mawakili wake, limeahirishwa hadi Septemba 16, 2026 kwa ajili ya kutajwa.

Shauri hilo lilitajwa leo Alhamisi, Julai 23, 2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma inayoketi Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, mbele ya Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Amir Mruma.

Katika mwenendo wa shauri hilo, Mkuu wa Gereza la Ukonga, ACP Andrew Shaban N'tamamiro, aliendelea na kukamilisha ushahidi wake kwa kujibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa waleta maombi pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Akitoa ushahidi wake mahakamani, ACP N'tamamiro alikiri kuwa aliwahi kuwachungulia mawakili wa Tundu Lissu walipokuwa wakizungumza na mteja wao gerezani, lakini alisisitiza kuwa hakuwahi kusikiliza mazungumzo yao.

Alieleza kuwa mlango wa chumba cha mazungumzo ulikuwa ukiachwa wazi kwa madhumuni ya kiusalama ili askari waweze kuwaona waliokuwemo ndani, na si kwa lengo la kusikiliza mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika.

Shahidi huyo pia alisema hafahamu kuwa Tundu Lissu aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mwaka 2017/2018, ingawa alikiri kuwafahamu mawakili Nashon Nkung na Paul Kisabo kutokana na ziara zao za mara kwa mara za kumtembelea Lissu gerezani.

Baada ya upande wa Jamhuri kukamilisha maswali ya ufafanuzi (re-examination), Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi Septemba 16, 2026, litakapoitwa tena kwa hatua nyingine.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم