MZAVA ATAKA MJADALA WA KITAIFA KUHUSU ONGEZEKO LA WATU NA MUSTAKABALI WA RASILIMALI ZA TANZANIA
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Utalii, Timothy Mzava, ameitaka Serikali na wadau mbalimbali kuanzisha mjadala mpana wa kitaifa kuhusu namna ya kuandaa Tanzania ya miaka 50 hadi 60 ijayo, kufuatia ongezeko kubwa la idadi ya watu linaloendelea kushuhudiwa nchini.
Mzava aliyasema hayo wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Wanyamapori, akieleza kuwa kasi ya ukuaji wa idadi ya watu inapaswa kuendana na mipango madhubuti ya maendeleo na uhifadhi wa rasilimali za taifa.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2002 Tanzania ilikuwa na takribani wananchi milioni 34, huku Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ikionesha idadi hiyo kufikia zaidi ya milioni 61, jambo linaloashiria ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma za kijamii, ardhi na matumizi ya rasilimali za asili.
“Maana yake ni kwamba idadi ya wananchi imeongezeka kwa kiwango kikubwa sana. Hivyo, kama taifa ni lazima tuwe na mjadala wa kina kuhusu namna ya kujenga Tanzania ya miongo ijayo. Bila kufanya hivyo tunaweza kujikuta tunakabiliana na changamoto kubwa zaidi siku zijazo,” alisema Mzava.
Alibainisha kuwa sekta za maliasili na utalii ni miongoni mwa maeneo yatakayoguswa zaidi na ongezeko la watu, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mikakati ya muda mrefu itakayohakikisha maendeleo ya wananchi yanaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.
Mzava alisema Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wake wana nafasi muhimu katika mjadala huo, hasa katika kutafuta njia bora za kulinda rasilimali za taifa huku zikichangia maendeleo ya wananchi.
“Sisi kama Bunge tuko tayari kushirikiana na Serikali katika mjadala huu ili kupata suluhisho la changamoto zinazoweza kujitokeza mbele ya safari. Lengo ni kuhakikisha tunalinda ustawi wa wananchi wetu na wakati huo huo tunahifadhi ustawi wa nchi yetu,” alisema.
Aidha, alimpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuimarisha uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za asili, akisisitiza kuwa matokeo ya sensa ya wanyamapori yatasaidia kupanga mikakati bora ya maendeleo ya sekta hiyo.
“Tunapokea taarifa hizi kwa umuhimu mkubwa kwa sababu zitasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu mustakabali wa maliasili na maendeleo ya taifa letu,” alisema Mzava.
Ends

Post a Comment