MILLYA AMUUNGA MKONO KIRIA LAIZER KUENDELEA KUONGOZA CCM SIMANJIRO
Na Joseph Ngilisho | SIMANJIRO
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya, ametangaza hadharani kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer, iwapo ataamua kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa chama unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.
Millya alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kama mgeni rasmi katika sherehe za kimila za jamii ya Kimasai zilizofanyika katika boma la Mzee Kurian Laizer wilayani Simanjiro, hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa chama na serikali, wazee wa mila, wafanyabiashara pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo
Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye sherehe hizo, Millya alisema Kiria ameonyesha uwezo mkubwa wa uongozi, amejenga mshikamano ndani ya chama na kushiriki kikamilifu katika kusukuma mbele agenda za maendeleo ya wananchi wa Simanjiro.
Alisema kutokana na utendaji wake, amejijengea sifa zinazomfanya kuwa mmoja wa viongozi wenye uwezo wa kuendelea kuimarisha chama na kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.
"Wakati ukifika wa uchaguzi wa chama mwaka 2027, mimi nitakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kusimama na kumuunga mkono Kiria Laizer. Ameonyesha uongozi wa vitendo, amekuwa karibu na wananchi na ana dhamira ya kweli ya kuwatumikia watu wa Simanjiro," alisema Millya huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria hafla hiyo.
Kauli hiyo imepokelewa kama ishara ya kuimarika kwa ushawishi wa Kiria ndani ya CCM wilayani Simanjiro, huku ikionyesha imani kubwa aliyonayo kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu wa chama na serikali.
Kiria, ambaye pia ni ndugu wa mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Saniniu Laizer, ameendelea kujijengea nafasi ya kisiasa ndani ya wilaya hiyo kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo na ushirikiano wake na wananchi.
"Nitaendelea kushirikiana na wananchi wa Simanjiro, kusikiliza kero zao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa maslahi ya jamii yetu," alisema Kiria.
Mbali na shughuli za kijamii, sherehe hizo za kimila za Kimasai zilitumika kuhamasisha umoja, kuhifadhi mila na desturi za jamii hiyo pamoja na kutoa nafasi kwa viongozi na wananchi kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo.
Wazee wa mila waliohudhuria hafla hiyo walisisitiza umuhimu wa viongozi kuendelea kushikamana na kuweka mbele maslahi ya wananchi ili kuimarisha maendeleo ya Simanjiro na kuhakikisha kizazi cha sasa na kijacho kinanufaika na matunda ya mshikamano huo.
Kauli ya Millya imeongeza mjadala wa kisiasa ndani ya Simanjiro, huku wengi wakiitafsiri kama ishara ya maandalizi ya mapema ya uchaguzi wa chama na mwelekeo wa siasa za eneo hilo kuelekea mwaka 2027.
Ends









Post a Comment