KAMATI YA BUNGE IKIONGOZWA NA DKT LUKUMAY YAISIFU BMH KWA HUDUMA ZA KIBINGWA BOBEZI, YATAKA UWEKEZAJI ZAIDI KWA MAGONJWA SUGU

KAMATI YA BUNGE YAISIFU BMH KWA HUDUMA ZA UBINGWA BOBEZI, YATAKA UWEKEZAJI ZAIDI KWA MAGONJWA SUGU

Na Joseph Ngilisho – Arushadigital | Dodoma


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, ikisema hospitali hiyo imeendelea kuwa tegemeo muhimu kwa wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanaohitaji matibabu maalumu.

Pongezi hizo zilitolewa Juni 9, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Johannes Lukumay, wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya hospitali hiyo, ikiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa Jengo la Saratani na tathmini ya huduma mbalimbali za kibingwa zinazotolewa.

Akizungumza baada ya kutembelea hospitali hiyo, Dkt. Lukumay alisema BMH imeonyesha mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za afya kutokana na uwekezaji wa Serikali pamoja na uongozi madhubuti wa Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Abel Makubi.

“Tumeshuhudia maendeleo makubwa ya miundombinu, teknolojia na huduma za matibabu. Hospitali hii imeendelea kujijengea heshima kubwa na kuwa miongoni mwa vituo vinavyoongoza nchini katika huduma za kibingwa na ubingwa bobezi,” alisema.

Alisema Kamati imevutiwa na kiwango cha huduma zinazotolewa pamoja na jitihada za watumishi wa hospitali hiyo katika kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora kwa wakati.


Dkt. Lukumay aliipongeza BMH kwa kuanzisha na kuendeleza huduma ya upandikizaji wa uloto (Bone Marrow Transplant), akibainisha kuwa tangu huduma hiyo ilipoanza mwaka 2023, watoto 30 wenye umri kati ya miaka minne hadi 12 wamefanikiwa kupatiwa matibabu hayo nchini, hatua iliyopunguza gharama kubwa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kugharamia matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza na sugu kama saratani, magonjwa ya moyo, figo, kisukari na mifupa, ili wananchi wengi zaidi waweze kupata huduma hizo kwa urahisi na kwa wakati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, alisema mafanikio yanayoshuhudiwa BMH yametokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya afya.

Alisema kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma za kibingwa 20 na huduma za ubingwa bobezi 17, jambo linaloifanya kuwa moja ya hospitali muhimu zaidi nchini katika utoaji wa matibabu maalumu.

“Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa hospitali hii kwa kuwekeza katika miundombinu, vifaa tiba vya kisasa na mafunzo ya wataalamu wa afya. Kupitia programu ya Samia Scholarship, wataalamu wengi wamepata nafasi ya kuongeza ujuzi na hivyo kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa,” alisema.

Dkt. Samizi alisema Serikali imetenga shilingi bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Saratani pamoja na shilingi bilioni nne kwa ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vitakavyoongeza uwezo wa hospitali hiyo katika kutoa huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali.

Aidha, aliwataka wananchi kuzingatia kanuni za afya na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yameendelea kuongezeka nchini.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, alisema hospitali hiyo imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma kwa wagonjwa, ikiwemo kupunguza muda wa kusubiri huduma kutoka siku mbili hadi tatu zilizokuwepo awali hadi wastani wa saa tatu hadi sita kwa sasa.

Alisema hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma mbalimbali za ubingwa na ubingwa bobezi, zikiwemo upasuaji wa moyo kwa watoto, upandikizaji wa figo, pamoja na matibabu ya magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Prof. Makubi alieleza kuwa BMH pia imeimarisha huduma kwa wateja kupitia kituo cha simu kinachofanya kazi saa 24 na mifumo ya kidijitali inayorahisisha mawasiliano kati ya wagonjwa na watoa huduma.

Aliongeza kuwa maabara ya hospitali hiyo imefanikiwa kupata ithibati ya kimataifa kwa mara ya tatu mfululizo, jambo linalothibitisha ubora wa huduma za uchunguzi zinazotolewa.


Kwa mujibu wa Prof. Makubi, BMH inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Figo chenye thamani ya shilingi bilioni 28 kwa ufadhili wa Serikali ya Japan, pamoja na maandalizi ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema kutokana na kupanuka kwa huduma na ongezeko la wagonjwa wanaohudumiwa kutoka ndani na nje ya nchi, hospitali hiyo inalenga kufikia hadhi ya Hospitali ya Taifa, hatua itakayoongeza zaidi uwezo wake wa kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa Watanzania.

***Ends***

Post a Comment

Previous Post Next Post