TEKNOLOJIA YA QR CODE YATAJWA KUWA MWAROBAINI WA UPOTEVU WA MAZAO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Teknolojia ya QR Code pamoja na matumizi ya akili unde (AI) imetajwa kuwa suluhisho muhimu litakalosaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa upotevu wa mazao na bidhaa za wakulima nchini huku ikiboresha mfumo wa uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji wa bidhaa hizo.
Wataalamu wa sayansi na teknolojia wamesema matumizi ya mifumo ya kisasa katika sekta ya kilimo yana uwezo mkubwa wa kuongeza tija kwa wakulima na kusaidia bidhaa zao kufuatiliwa kwa urahisi kutoka shambani hadi sokoni.
Akizungumza katika Kongamano la NAIC linaloendelea jijini Arusha Mei 19, 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Haroun Makandi alisema dunia ya sasa haihitaji tena kilimo cha mazoea bali kinachoendeshwa kwa kutumia teknolojia.
Alisema teknolojia ya QR Code (msimbo milia) inaweza kusaidia kufuatilia mazao au bidhaa za wakulima kutoka eneo moja hadi jingine, jambo litakalosaidia kudhibiti upotevu wa mazao pamoja na kuongeza uaminifu wa bidhaa hizo sokoni.
“Tunapozungumzia kilimo cha kisasa tunazungumzia matumizi ya AI na QR Code. Hii ni teknolojia inayoweza kufuatilia bidhaa kuanzia uzalishaji hadi zinapomfikia mlaji,” alisema Dk. Makandi.
Alifafanua kuwa mfumo wa precision farming unaotumia teknolojia kama GPS, vitambuzi na uchambuzi wa taarifa umeendelea kuleta mapinduzi makubwa katika uzalishaji wa mazao kwa kutumia rasilimali chache lakini kwa matokeo makubwa zaidi.
“Sasa hivi sio suala la kulima tu na kumwagilia maji. Teknolojia ndiyo inaelekeza kiwango sahihi cha matumizi ya maji, mbolea na huduma nyingine zinazohitajika katika uzalishaji,” alisema.
Aidha alisema changamoto kubwa inayowakabili wakulima wengi ni namna ya kuhifadhi na kusafirisha mazao yao, hali inayochangia upotevu mkubwa baada ya mavuno.
“Tunapozungumzia logistics, tunazungumzia kuvuna, kuhifadhi, kusafirisha na kuuza mazao. Upotevu mkubwa unatokana na ukosefu wa mifumo bora ya kufuatilia bidhaa hizo,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Makandi, matumizi ya QR Code yanaweza pia kutoa mrejesho wa haraka kwa wazalishaji kuhusu ubora wa bidhaa zao pamoja na mwenendo wa soko.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Scan Code Tanzania, Faustine Mgimba alisema matumizi ya teknolojia yanapaswa kuwafikia wananchi wote ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika mapinduzi ya kidijitali.
Alisema dhamira ya kampuni hiyo ni kuhakikisha teknolojia inatumika kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi, hususan katika kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za ndani.
“Kama taifa tunapaswa kutumia teknolojia kama chachu ya maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi wetu,” alisema Mgimba.







إرسال تعليق