SERIKALI YATOA ONYO KALI DHIDI YA WANAOTUMIA MITANDAO KUCHOCHEA NA KUIDHALILISHA NCHI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imetoa onyo kali kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza matusi, uchochezi na taarifa za upotoshaji dhidi ya serikali pamoja na viongozi wake, ikisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa bila kusita kwa wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Homera wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali yaliyofanyika jijini Arusha, ambapo amesema tayari serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya wahusika wanaotumia majukwaa ya kidijitali kuvuruga amani na mshikamano wa taifa.
Dk Homera alisema orodha ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo tayari imewasilishwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi kupitia Jeshi la Polisi.
Alisema serikali haitakubali kuona uhuru wa maoni ukitumika kama silaha ya kutukana viongozi, kuchafua taswira ya nchi na kuchochea taharuki miongoni mwa wananchi kupitia taarifa zisizo na ukweli.
“Uhuru wa kutoa maoni upo, lakini usitumike kuvunja sheria, kuchochea vurugu au kudhalilisha wengine,” alisema Dk Homera.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, aliwataka mawakili wa serikali kuwa mstari wa mbele katika kupambana na upotoshaji wa taarifa unaofanyika mitandaoni kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa.
Dk Ndumbaro alisema matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamekuwa yakihatarisha maadili, kuvuruga utulivu wa jamii na kupunguza imani ya wananchi kwa taasisi za serikali, hali inayopaswa kudhibitiwa kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuhakikisha matumizi ya mitandao ya kijamii yanafanyika kwa kuzingatia sheria, maadili na kulinda amani pamoja na usalama wa nchi.
Ends..

إرسال تعليق