WARAKA WA PILI WA SABINA JOHN AANIKA MAISHA YAKE YA MATESO NA MAFANIKIO YA MABILIONI,AHITAJI MSAADA WA HALI NA MALI

 WARAKA WA PILI WA SABINA JOHN AANIKA MAISHA YAKE YA MATESO NA MAFANIKIO YA MABILIONI

Na SABINA JOHN 
 

MWANAMKE anayefahamika kwa jina la Sabina John ameibuka na kuandika waraka wake wa pili uliojaa simulizi nzito ya maisha yake, akifunguka kuhusu safari yake kutoka maisha ya umaskini hadi kufikia mafanikio makubwa ya biashara yaliyomwezesha kumiliki magari 11 ya biashara, nyumba tano, viwanja, silaha halali pamoja na fedha zinazodaiwa kuzidi Sh bilioni mbili zilizofungiwa benki kwa zaidi ya miaka minne wakati kesi mbalimbali zikiendelea.

Katika waraka huo, Sabina John alisema mali zote anazomiliki ni halali na zimetokana na biashara na juhudi zake binafsi pamoja na familia yake.
Alisema licha ya mafanikio hayo, maisha yake yalibadilika na kuwa ya mateso kufuatia kukumbwa na maradhi, madeni, migogoro, kuibiwa, kufungwa pamoja na kuishi maisha ya kujificha maporini kwa hofu ya usalama wake.

“Baada ya maradhi, madeni, migogoro, kuibiwa na kufungwa, niliishi maisha ya hatari maporini nikijificha kuepuka madhara mengi,” alisema Sabina John katika waraka huo.
Sabina alimshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuendelea kuwa hai huku akisema amepewa hekima, akili na kibali cha kuendelea kusimama licha ya changamoto alizopitia.

Pia aliwashukuru wanafamilia, jamii, vyombo vya habari pamoja na taasisi za haki za binadamu kwa kumpa faraja na matumaini ya kupata haki zake zote.

Katika waraka huo, Sabina aliwataja marafiki zake kutoka England na London, ANTHON GORDONS na KRISTIAN KHALID, akisema wamekuwa wakipitia mateso nchini kwa muda mrefu baada ya kudhulumiwa katika madai yanayofikia zaidi ya Sh milioni 500.

Hata hivyo alikishukuru sana kituo cha Sheria na haki za binadamu mkoani Arusha kwankujitolea kunisaidia kuendesha kesi zangu bure na kujihakikishia kupigania haki zangu pega kwa bega.

Alisema kupitia ushirikiano na wakili wake Bonifasi Gobero wa Tanganyika Law pamoja na taasisi za Mama Samia Legal Aid na TAULA, ameendelea kupata ushauri na mwongozo wa kisheria katika kufuatilia haki zake.

ASIMULIA ALIVYOANZA MAISHA YA BIASHARA
Sabina John alisema alizaliwa Sanya Juu mkoani Kilimanjaro katika familia ya John Mosi na Joyce Kimaro.

Alisema baada ya kuhitimu elimu ya sekondari alijiunga na Chuo cha Ualimu Tanga Eckernford mwaka 2003 lakini alishindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa ada na mahitaji muhimu.
Kutokana na changamoto hizo, alisema alihamia Arusha akiwa na miaka 17 kutafuta maisha huku akiwa hana makazi wala msaada wa ndugu kwa hofu ya kurudishwa kijijini.

“Niliishi maisha ya mitaani. Nilianza biashara kwa mtaji wa Sh8,000 nikitembea kuuza nguo, viatu, vipodozi na bidhaa za urembo hadi nilipopata mafanikio,” alisema.

Alisema baadaye aliamua kuolewa akiwa na miaka 18 ili kupata mwenza wa kushirikiana naye katika maisha.

Sabina alisema aliendelea na elimu ya chuo na kupata cheti kilichomwezesha kufundisha katika shule mbalimbali ikiwemo Lucky Vincent na Kilimanjaro kabla ya kujikita zaidi katika biashara.

Kwa mujibu wa Sabina, aliendesha biashara ya vipodozi, mavazi, mazao pamoja na usambazaji wa bidhaa kutoka Uganda, Nairobi na Afrika Kusini kwa wafanyabiashara mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha alisema aliingia katika biashara ya mazao kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo NMC, Mrombo, Mbauda pamoja na nchi jirani.
Sabina alisema mafanikio makubwa zaidi yalikuja baada ya kuingia kwenye biashara ya magari yaliyotumika.

“Nilinunua gari langu la kwanza aina ya Corolla. Nilipopata faida nilinunua Vitz, baadaye IST na kuendelea kushirikiana na madalali wa magari katika kuuza na kununua magari Dar es Salaam, Tanga na mikoa mingine,” alisema.

AELEZA MISAADA YA KIJAMII ALIYOTOA
Katika waraka huo, Sabina alisema mbali na biashara, aliwahi kutoa ushauri nasaha kwa waraibu wa dawa za kulevya, watu waliokata tamaa pamoja na vijana zaidi ya 300.

Alisema pia alikuwa akitoa sadaka katika nyumba za ibada, kulipa kodi za serikali, kusaidia wazazi, wakwe, ndugu pamoja na wananchi wasiokuwa na uwezo kwa kuwapatia chakula, mavazi, malazi, ada za shule na mitaji ya biashara.

“Niliwahi kujisahau binafsi kwa ajili ya kusaidia wengine. Wengine waliona kama nimechanganyikiwa lakini ilikuwa ni nadhiri na msukumo wa moyo wangu,” alisema.

Aidha alisema alikuwa akitembelea magereza na hospitali kila Jumapili kutoa misaada na faraja bila kujitangaza.

Sabina alisema historia hiyo ndiyo iliyosababisha yeye kuaminiwa kuwa msimamizi wa mali za familia ya Mzee Ally na Bi Fatma Mwase katika kesi ya mirathi iliyodumu kwa zaidi ya miaka minne.

ATOA WITO WA MSHIKAMANO NA HAKI
Katika waraka wake huo wa pili, Sabina John alisema ana matumaini ya kupata haki, ulinzi, huduma za afya, makazi ya kudumu pamoja na mazingira salama ya maisha.

Pia alitangaza mpango wa kuanzisha taasisi za NURU na MELITA HOPE zitakazolenga kusaidia watu wasiokuwa na uwezo kupitia huduma za kijamii na msaada wa kisheria.

Sabina alisema taasisi hizo zitajikita katika kuhamasisha upendo, amani, umoja, kusaidia wananchi kupata fursa za kiuchumi, kuongeza thamani ya rasilimali za Tanzania pamoja na kutoa elimu ya kupambana na changamoto za maisha.

“Tukishirikiana na viongozi wa serikali, dini na jamii, inawezekana kuona hakuna anayekosa chakula, makazi, elimu, afya na haki za msingi,” alisema Sabina John.
Ends.

Post a Comment

أحدث أقدم