DC KARATU AWEKA MSIMAMO MGOGORO MWEKEZAJI NA MPANGAJI MANYARA SAFARI LODGE, ATOA WIKI MBILI KWA SULUHU YA KISHERIA
Na Joseph Ngilisho | KARATU
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, ameweka msimamo wa serikali kwa kuingilia kati mgogoro wa upangaji katika Manyara Safari Lodge, akitoa muda wa wiki mbili kwa pande zinazohusika kumaliza tofauti zao kupitia vyombo vya sheria huku akisisitiza kwa msisitizo mkubwa kulindwa kwa taswira ya taifa, sekta ya utalii na usalama wa wageni.
Akizungumza kuhusu mgogoro huo, Karanga alisema serikali imechukua hatua hiyo mahsusi ili kuzuia athari zozote kwa wageni na uchumi wa utalii, akionya kuwa haitavumilia hali yoyote itakayovuruga amani au kuharibu sura ya Tanzania, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inajiandaa kupokea wageni wengi wa kimataifa kuelekea mashindano ya AFCON.
“Tusioneshe migogoro yetu kwa wageni. Heshima ya nchi iko juu. Wageni waendelee kuhudumiwa wakati pande husika zikiendelea na taratibu za kisheria,” alisema Karanga.
Kwa mujibu wa maelekezo hayo, mpangaji wa lodge hiyo ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake kwa muda wa wiki mbili ili kukamilisha huduma kwa wageni waliokwisha fanya booking na wanaotarajiwa kuwasili, kabla ya hatua za kisheria kuchukua mkondo wake rasmi baada ya kipindi hicho.
Karanga alisisitiza kuwa uamuzi huo ni wa mpito na haumaanishi kumpa ushindi upande wowote, bali ni kulinda maslahi mapana ya taifa, kuhakikisha utulivu unaendelea kuwepo na huduma za hoteli haziathiriki wakati mgogoro huo ukipatiwa suluhu kupitia mifumo halali ya kisheria. Aliongeza kuwa pande zote zinapaswa kutumia diplomasia ya kibiashara na kuepuka migogoro ya hadharani inayoweza kuathiri taswira ya nchi.
Aidha, alieleza kuwa serikali inafuatilia kwa karibu mgogoro huo na kusisitiza kuwa utatatuliwa kwa njia za kisheria bila kuingilia uhuru wa vyombo vya haki, huku akitoa wito kwa wawekezaji kuendelea kuwa na imani na mifumo ya kisheria ya nchi.
Hatua hiyo ya serikali imekuja kufuatia mgogoro kati ya mwekezaji wa kampuni ya Tarylin Ltd, Timothy Flavell, na mpangaji wake Erick Mashauri ambapo mwekezaji anamdai Mashauri kiasi Cha dola milioni 26 baada ya kushindwa kumlipa kwa muda mrefu na kuamua kusitisha mkataba wake kwa kumtaka aondoke.
Kwa ufupi, mwekezaji huyo amelalamikia kile alichodai kuwa ni ukiukwaji wa mkataba wa upangaji, akidai kuwa mkataba ulisitishwa rasmi Aprili 1, 2026 baada ya madai ya deni la pango, huku juhudi za kumtaka mpangaji kuondoka zikishindikana licha ya notisi kadhaa.
Flavell pia aliiomba serikali iingilie kati kulinda uwekezaji wake, akidai kufuata taratibu zote za kisheria bila mafanikio.
Hata hivyo, msimamo wa Mkuu wa Wilaya umeelekeza kuwa suluhu ya kudumu itapatikana kupitia vyombo vya sheria baada ya kipindi hicho cha mpito.
Mgogoro huo unaendelea kufuatiliwa huku ukiibua mjadala mpana kuhusu ulinzi wa mikataba ya kibiashara na umuhimu wa kudumisha mazingira rafiki ya uwekezaji nchini bila kuathiri sekta nyeti ya utalii.





0 Comments