WAONGOZA WATALII 2,000 WAPIGWA MSASA ARUSHA, SERIKALI, SEKTA BINAFSI NA TATO WAUNGANISHA NGUVU KUBORESHA UTALII

WAONGOZA WATALII 2,000 WAPIGWA MSASA ARUSHA, SERIKALI, SEKTA BINAFSI NA TATO WAUNGANISHA NGUVU KUBORESHA UTALII

 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


SERIKALI ,sekta binafsi na wadau wa utalii nchini wameungana kuimarisha ubora wa huduma katika sekta ya utalii, baada ya jumla ya waongoza watalii 2,000 kuanza mafunzo maalum jijini Arusha yanayolenga kuongeza taaluma, usalama wa wageni na ushindani wa kimataifa.



Akifungua rasmi mafunzo hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alisisitiza kuwa waongoza watalii ni kiungo muhimu katika mafanikio ya sekta hiyo, akiwataka kuwa mabalozi wa kweli wa Tanzania kwa kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wageni.


“Nyinyi ndio uso wa kwanza wa nchi yetu kwa watalii. Jinsi mnavyowahudumia ndivyo inavyojenga au kubomoa taswira ya Tanzania kimataifa,” alisema Dkt. Kijaji.


Alieleza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya utalii yanatokana na juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan kupitia kampeni za kimkakati za kuitangaza Tanzania duniani kama The Royal Tour na Amazing Tanzania.



Kwa mujibu wa Waziri huyo, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 161 kati ya mwaka 2021 hadi 2025, huku mapato ya sekta hiyo yakiongezeka kwa asilimia 238.5—hatua aliyoeleza kuwa ni ishara ya kukua kwa sekta hiyo na mchango wake kwa uchumi wa taifa.


Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kulindwa kupitia uwekezaji katika rasilimali watu, akibainisha kuwa mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa kushirikiana na Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO) ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ubora wa huduma na ushindani wa Tanzania kimataifa.


Dkt. Kijaji alisema mafunzo hayo yanaendana na malengo ya Serikali ya kufikia watalii milioni nane na kuongeza mchango wa utalii katika Pato la Taifa hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2030.


Aliongeza kuwa kaulimbiu ya mafunzo hayo, “Utaalamu, Usalama na Uongoza Watalii Wenye Uwajibikaji katika Maeneo ya Hifadhi Tanzania,” inalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kukabiliana na changamoto za kazi zao, hususan katika maeneo ya hifadhi.


Aidha, aliwakumbusha waongoza watalii umuhimu wa kuzingatia usalama wa wageni na kufuata taratibu za hifadhi, akisisitiza kuwa wanabeba dhamana ya maisha ya watalii na uhifadhi wa rasilimali za taifa.


“Ni lazima muwe na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa haraka. Usalama wa wageni ni kipaumbele, lakini pia tunalinda urithi wetu wa asili kwa vizazi vijavyo,” alisisitiza.


Waziri huyo pia alieleza kuwa Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kimataifa, yakiwemo Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards Grand Final 2026) na mashindano ya AFCON 2027, akitaja matukio hayo kama fursa muhimu ya kukuza utalii.


Aliwataka wadau kuanza maandalizi mapema kwa kubuni vifurushi maalum vya utalii vitakavyowavutia wageni, ili kunufaika kikamilifu na ujio wa wageni wa kimataifa.


Kwa upande wa sekta binafsi, kampuni ya Zara Tours imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha ubora wa huduma na kukuza taswira ya Tanzania kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo, Mkurugenzi wake, Zainabu Ansell, alisema mafanikio ya sekta ya utalii yanatokana na ushirikiano thabiti kati ya Serikali na sekta binafsi, huku akisisitiza umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wanaohudumia wageni moja kwa moja.


“Haya ni mafunzo muhimu sana. Tunapoongelea utalii bora, tunazungumzia kuwajengea uwezo wale wanaokutana moja kwa moja na wageni wetu. Hii itaongeza ubora wa huduma na kuimarisha taswira ya nchi yetu,” alisema.


Aliongeza kuwa Zara Tours itaendelea kuwekeza katika rasilimali watu na ubunifu wa huduma ili kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanapata uzoefu bora na kuwa mabalozi wazuri wa nchi hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TATO, Elirehema Maturo, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waongoza watalii na madereva ili waweze kukidhi ushindani wa soko la kimataifa.


Alibainisha kuwa mafunzo hayo yanakuja wakati muafaka, yakilenga kuboresha huduma kwa kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza katika misimu iliyopita ya utalii.


“Utalii ni biashara ya kimataifa. Tusipokuwa na ushindani wa kutosha, tutapoteza nafasi yetu. Ndiyo maana ni lazima tuendelee kuboresha ubora wa huduma kila wakati,” alisema Maturo.


Aliongeza kuwa programu hiyo pia ni jukwaa la wadau kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto za kiutendaji, hasa katika kipindi cha msimu wa chini wa utalii.


Maturo alisisitiza kuwa TATO itaendelea kuandaa mafunzo kama hayo na kupanua wigo wake ili kufikia wadau wengi zaidi nchini, akibainisha kuwa ubora wa huduma ndio msingi wa ushindani wa Tanzania katika soko la utalii duniani.


Kwa ujumla, mafunzo hayo yanaonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya utalii nchini, huku wadau wakisisitiza kuwa uwekezaji katika ujuzi na taaluma ya waongoza watalii ni nguzo kuu ya mafanikio ya muda mrefu ya sekta hiyo.


ENDS..

Post a Comment

0 Comments