UNESCO, MAIPAC WAJA NA MWONGOZO KULINDA JAMII ZA PEMBEZONI DHIDI YA UNYONYAJI WA MAUDHUI

 UNESCO, MAIPAC WAANDAA MWONGOZO WA MAUDHUI KULINDA JAMII ZA PEMBEZONI

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari inayosaidia jamii za pembezoni (MAIPAC) pamoja na Idara ya Habari – Maelezo, wameanza maandalizi ya mwongozo maalum utakaowaongoza wanahabari na watengeneza maudhui wanapofanya kazi katika jamii za pembezoni.

Mwongozo huo unalenga kuweka misingi ya maadili na weledi katika uandaaji na usambazaji wa maudhui kuhusu jamii za asili ikiwemo Wahadzabe, Wamasai, Wadatoga na Waakie, ili kulinda heshima, mila na utamaduni wao.


Akizungumza jijini Arusha jana katika mjadala wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma, alisema hatua hiyo inakuja kufuatia ongezeko la watengeneza maudhui wanaoingia katika jamii hizo bila kufuata maadili ya taaluma.

Alisema baadhi ya watengeneza maudhui, wa ndani na nje ya nchi, wamekuwa wakichukua picha na taarifa kutoka kwa jamii hizo bila ridhaa yao, huku baadhi ya maudhui hayo yakikiuka mila, desturi na utu wa jamii husika.

“Kwa kutambua changamoto hii, MAIPAC kwa kushirikiana na UNESCO na Idara ya Habari – Maelezo tunaandaa mwongozo maalum utakaosaidia kazi za uandishi na utengenezaji maudhui katika jamii hizi kufanyika kwa kuzingatia maadili na heshima,” alisema Juma.

Aliongeza kuwa, pamoja na mwongozo huo, taasisi hizo kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo SAVVY Media, zinatarajia kuwajengea uwezo wanajamii hao katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili waweze kunufaika kiuchumi kupitia maudhui yao.

“Tutahakikisha jamii hizi zinapata elimu ya matumizi ya mitandao, zinatambua haki zao za kidigitali na kutumia fursa zilizopo kuinua uchumi wao,” alisisitiza.

Katika mjadala huo, baadhi ya watengeneza maudhui na maafisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), walieleza kuwa matumizi ya teknolojia ikiwemo akili unde (AI) yanapaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa vijana na jamii, badala ya kuleta hofu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jamii ya Wahadzabe katika Bonde la Eyasi, wilayani Karatu, Mdindi Samboga, aliipongeza hatua hiyo akisema itasaidia jamii yao kunufaika na uwepo wao kwenye majukwaa ya kidigitali.

Alisema licha ya jamii hiyo kupata umaarufu mkubwa mitandaoni, bado wanajamii hawapati faida stahiki kutokana na maudhui yanayotengenezwa kuhusu maisha yao.

“Wanakuja wanatupiga picha na kutuhoji, tunasikia mijini tunaonekana sana, lakini sisi hatuoni faida yoyote zaidi ya kupewa vitu visivyo na thamani. Tunaomba sasa tusaidiwe kunufaika,” alisema Samboga.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni muhimu katika kuhakikisha jamii za pembezoni zinalindwa dhidi ya unyonyaji wa maudhui, huku zikipewa nafasi ya kushiriki na kunufaika katika uchumi wa kidigitali.





MWISHO

Post a Comment

0 Comments