MWENYEKITI WA KAMATI ASISITIZA UMUHIMU WA CHANJO, SERIKALI YAONGEZA NGUVU HUDUMA ZA AFYA
Na Joseph Ngilisho | PWANI
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay, amesisitiza umuhimu wa chanjo kama nguzo kuu ya kulinda afya ya jamii na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, hususan kwa watoto chini ya miaka mitano.
Akizungumza kwa msisitizo katika Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kimataifa 2026 yaliyofanyika Kibiti mkoani Pwani, Dkt. Lukumay ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi,alisema Serikali imeongeza nguvu katika utoaji wa huduma za chanjo ili kuhakikisha wananchi wote wanapata kinga dhidi ya magonjwa hatarishi.
Alieleza kuwa chanjo si tu huduma ya afya, bali ni uwekezaji muhimu kwa maendeleo ya taifa, kwani husaidia kupunguza mzigo wa magonjwa, gharama za matibabu, na kuongeza tija ya nguvu kazi ya wananchi.
“Chanjo ni haki ya msingi kwa kila mtoto na ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha mtoto anapata chanjo zote kwa wakati. Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,” alisisitiza.
Dkt. Lukumay alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa chanjo mbalimbali, ikiwemo chanjo ya homa ya ini, sambamba na kuendeleza huduma za chanjo za kawaida ili kuwafikia watoto waliokosa chanjo kwa wakati.
Aliongeza kuwa juhudi za kuwafikia wananchi katika maeneo ya vijijini na pembezoni zimeongezwa kupitia huduma za mkoba na kampeni maalum za uhamasishaji, hatua inayolenga kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa huduma za afya.
Aidha, alisisitiza kuwa utoaji wa chanjo bure utaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali, akieleza kuwa hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano nchini.
“Hatua hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha sekta ya afya na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora na salama,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliwataka wazazi na walezi kupuuza taarifa potofu kuhusu chanjo na badala yake kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya ili kulinda maisha ya watoto na jamii kwa ujumla.
Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kimataifa 2026 yamekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kinga dhidi ya magonjwa, huku wadau wa afya wakisisitiza ushirikiano wa pamoja katika kufanikisha malengo ya afya bora kwa wote.
Ends.

0 Comments