DARTS YAANZA KUNG’ARA ARUSHA, YAPATA MSUKUMO MPYA KUELEKEA AFCON 2027

 DARTS YAANZA KUNG’ARA ARUSHA, YAPATA MSUKUMO MPYA KUELEKEA AFCON 2027

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA

Afisa Utamaduni na Michezo wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, amesema jiji hilo linaendelea kujiimarisha katika sekta ya michezo kwa kuibua vipaji vipya kupitia michezo mbalimbali, ikiwemo mchezo wa darts, ambao unaanza kupata umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana.

Akizungumza jana baada ya kufunga mashindano makubwa ya darts yaliyofanyika jijini hapa, Maneno alisema mashindano hayo ni sehemu ya maandalizi ya mashindano ya UMOJA Cup yanayotarajiwa kushirikisha nchi za Kenya na Tanzania.

Alisema kuwa Arusha ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha kukuza michezo kuelekea michuano ya AFCON 2027, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia michezo kama darts kama chachu ya kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika matukio ya michezo ya kimataifa.

“Tunataka kuona darts inakuwa sehemu ya michezo inayotambulika na kufundishwa kuanzia ngazi ya chini kabisa, hasa mashuleni, ili kuibua vipaji vya watoto mapema,” alisema Maneno.

Aidha, alitoa wito kwa chama cha mchezo huo kuandaa mipango madhubuti ya kuanzisha programu maalum za kufundisha darts mashuleni, hatua itakayosaidia kukuza mchezo huo na kuwajengea watoto nidhamu, umakini pamoja na ushindani wa kimataifa.

Kwa mujibu wa Maneno, uwekezaji katika michezo ya aina mbalimbali ni njia mojawapo ya kuandaa kizazi cha wanamichezo kitakachoweza kuiwakilisha Tanzania kimataifa, sambamba na kuimarisha afya na ajira kwa vijana.

Mashindano hayo yameacha gumzo jijini Arusha, huku wadau wa michezo wakiamini kuwa darts inaweza kuwa miongoni mwa michezo itakayokuja kwa kasi na kuleta ushindani mkubwa katika siku zijazo.




Ends..

Post a Comment

0 Comments