MADUDU HOSPITALI YA ALMC -SELIAN ARUSHA: MWILI WA MEREHEMU WABADILISHWA NDUGU WAZIKA MWINGINE MTIFUANO MKALI WAIBUKA

MKANGANYIKO MOCHWARI: MWILI WA MAREHEMU WABADILISHWA ALMC (SELIAN), ARUSHA

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA

Hali ya sintofahamu imeibuka katika Hospitali ya ALMC (maarufu Selian), jijini Arusha, kufuatia madai ya kubadilishwa kwa miili ya marehemu wawili, tukio lililosababisha mshtuko na maswali mengi juu ya umakini wa hospitali hiyo

Inadaiwa kuwa mwili wa marehemu Mzee Rubeni Pallangyo (74) ulichanganywa na mwili wa marehemu mwingine aliyefahamika kwa jina la Talalai, hali iliyosababisha familia moja kudai kumzika mtu ambaye si ndugu yao bila kufahamu.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu Pallangyo, walifika katika chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari) asubuhi kwa lengo la kuchukua mwili wa mpendwa wao kwa ajili ya kuuaga katika eneo la Sekei kabla ya mazishi yaliyopangwa kufanyika wilayani Arumeru. Hata hivyo, walishangazwa kukuta mwili huo haupo.

“Tulipofika mochwari hatukuukuta mwili wa baba yetu. Tukaelezwa kuwa tayari ulizikwa jana na familia nyingine,” alieleza mmoja wa ndugu kwa masikitiko makubwa.

Taarifa zinaeleza kuwa familia nyingine ilifanya mazishi katika eneo la Sanawari (Maduka Matatu) siku iliyotangulia, bila kufahamu kuwa waliuzika mwili wa Mzee Pallangyo badala ya ndugu yao halisi.

Mzee Pallangyo alifariki dunia Alhamisi, Aprili 2, 2026, na maandalizi yote ya mazishi yalikuwa tayari yamekamilika kabla ya kubainika kwa mkanganyiko huo.

Juhudi za kuwasiliana na uongozi wa Hospitali ya ALMC (Selian) ili kutoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo hazikufanikiwa. Aidha, jitihada za kumpata kiongozi wa hospitali hiyo aliyetajwa kwa jina la Dkt. Saleh hazikuzaa matunda, baada ya mara kwa mara kuelezwa kuwa yupo kwenye majukumu ya kuwahudumia wagonjwa.

Tukio hili limeibua maswali mazito kuhusu mifumo ya utambuzi na uhifadhi wa miili katika mochwari, hususan namna ambavyo majina na namba za utambulisho zinavyoweza kuchanganywa hadi kusababisha mazishi ya mtu asiyehusika.

Wadau mbalimbali wanahoji iwapo taratibu za mwisho za utambuzi wa miili kabla ya mazishi zilifuatwa ipasavyo, na kama familia iliyofanya mazishi ilipata fursa ya kuthibitisha mwili wa marehemu wao.

Uchunguzi zaidi unatarajiwa kufanyika ili kubaini chanzo cha tatizo hilo na kuwawajibisha wahusika, huku familia zote zilizoathirika zikisubiri haki na ufafanuzi wa kina juu ya tukio hilo.

Ends..

Post a Comment

0 Comments