TANROADS YAOMBA BILIONI 20 KUWEKA TAA BARABARA ZA ARUSHA
Na Joseph Ngilisho |ARUSHA
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeomba kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya mradi wa uwekaji taa katika barabara kuu za Jiji la Arusha pamoja na barabara ya mzunguko (bypass) ya Ngaramtoni, hatua inayolenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara, kupunguza ajali pamoja na kuboresha mandhari ya jiji hilo linalokua kwa kasi kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Regnard Masawe, alisema taasisi hiyo imewasilisha serikalini ombi la fedha hizo kwa ajili ya kufunga taa katika barabara zote muhimu ndani ya jiji, pamoja na barabara ya mzunguko ya Ngaramtoni kuelekea Uwanja wa Ndege wa Arusha na barabara ya Arusha–Moshi.
Alisema tayari serikali imepokea na kukubali ombi hilo, hatua inayotarajiwa kuharakisha utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kuboresha miundombinu ya barabara katika jiji hilo.
“Tumewasilisha serikalini ombi la takribani shilingi bilioni 20 ili kuwezesha uwekaji wa taa katika barabara zote za Jiji la Arusha pamoja na barabara ya bypass ya Ngaramtoni. Lengo ni kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara hasa nyakati za usiku na kurahisisha usafiri kwa wananchi,” alisema Masawe.
Alieleza kuwa uwekaji wa taa hizo pia ni sehemu ya maandalizi ya kuboresha miundombinu ya jiji hilo kuelekea mashindano ya Africa Cup of Nations, ambapo Tanzania inatarajia kuwa miongoni mwa nchi zitakazoshiriki maandalizi na shughuli mbalimbali zitakazoambatana na mashindano hayo ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Masawe, kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara na taa kutasaidia kuongeza usalama wa wageni na watalii watakaotembelea jiji la Arusha wakati wa mashindano hayo, pamoja na kuimarisha taswira ya jiji hilo kama lango la utalii na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha, alisema mradi huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi katika jiji la Arusha kwa kuwezesha usafiri kuwa salama na rahisi muda wote wa siku na usiku, hali itakayochochea ukuaji wa biashara, utalii na uwekezaji.
Masawe aliongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaenda sambamba na juhudi nyingine za kuboresha miundombinu ya barabara mkoani humo, ikiwemo ukarabati na upanuzi wa baadhi ya barabara kuu zinazounganisha maeneo mbalimbali ya jiji na viunga vyake.
Katika hatua nyingine, Masawe alieleza changamoto kadhaa zinazokabili barabara zinazosimamiwa na wakala huo, ikiwemo utupaji holela wa taka ngumu katika hifadhi ya barabara pamoja na uvamizi wa maeneo ya akiba ya barabara.
Alisema hali hiyo imekuwa ikichangia kuathiri matumizi sahihi ya barabara na kusababisha msongamano pamoja na hatari kwa watumiaji wa miundombinu hiyo.
Aliwataka viongozi wa halmashauri kushirikiana kwa karibu na TANROADS kudhibiti tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wadogo kuvamia maeneo ya barabara kwa kupanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara, ikiwemo kutumia mikokoteni, jambo linalosababisha kupungua kwa upana wa barabara na wakati mwingine kuathiri upitishaji wa magari hasa nyakati za jioni.
Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa serikali walisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya barabara pamoja na kushiriki katika kampeni za usafi wa mazingira ili kuhakikisha maendeleo ya miundombinu yanaendana na mandhari safi ya jiji.
Hatua za kuboresha miundombinu ya barabara, ikiwemo uwekaji wa taa, zinatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri, usalama barabarani na maendeleo ya kiuchumi katika Jiji la Arusha na maeneo yanayolizunguka.
Ends..







0 Comments