ZARA TOURS YA MOSHI YANG’ARA TENA SERENGETI AWARDS, YAENDELEZA MSHIKAMANO WA TUZO ZA KIMATAIFA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Tuzo hiyo ni miongoni mwa tuzo 51 zilizotolewa katika hafla kubwa ya Serengeti Awards, ambapo Kampuni ya Kitalii ya Zara Tour iliyoibuka kidedea katika Kategori ya Kampuni bora ya Utalii Kanda ya Kaskazini (Best Tour Operator Northern zone) katika Usiku wa Tuzo za “The Serengeti Awards” zilizofanyika Januari 31,2026, katika Ukumbi wa Mount Meru Hotel- Arusha.
iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika Hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha, hafla iliyowakutanisha wadau wakuu wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye aliipongeza sekta ya utalii kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa, kuongeza ajira na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Zara Tours, Bi. Zainabu Ansell, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa, mshikamano wa timu na ushirikiano mzuri kati ya serikali na wadau wa sekta ya utalii, hususan katika kulinda na kuendeleza vivutio vya Taifa kama Mlima Kilimanjaro.
“Mafanikio yanayoonekana katika Mlima Kilimanjaro ni ushahidi wa wazi wa kazi kubwa iliyofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya utalii. Mazingira ya mlima yameimarika, huduma zimeboreshwa na hali ya usalama imeongezeka kwa kiwango kikubwa, jambo linalowapa watalii uzoefu wa kipekee,” alisema Bi. Zainabu.
Aliongeza kuwa kupitia maboresho hayo, Mlima Kilimanjaro umeendelea kuitangaza Tanzania kimataifa, na kuifanya nchi kuwa moja ya vituo vinavyoongoza kwa utalii wa mlima barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, ongezeko la watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro limechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii na kuongeza mapato ya Taifa, huku kampuni kama Zara Tours zikichukua nafasi muhimu katika kuhakikisha wageni wanapata huduma zenye viwango vya kimataifa.
“Ninajivunia sana mafanikio haya, na leo ni siku ya kusherehekea hatua tulizofikia. Mimi pamoja na timu yangu tumejipanga kikamilifu kuendelea kuboresha viwango vya kitaaluma, kuongeza ubunifu na kuhakikisha wageni wengi zaidi wanavutiwa kuja kuupanda Mlima Kilimanjaro,” alisisitiza.
Bi. Zainabu aliahidi kuwa Zara Tours itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kukuza utalii endelevu, kulinda mazingira, na kulitangaza Taifa la Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.
Hafla ya Serengeti Awards imelenga kutambua na kuthamini mchango wa taasisi, makampuni na watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Ends..




0 Comments