HALMASHAURI YAFUNGUKA MAZITO:
YAKANUSHA UPOTOSHAJI, YAFICHUA MADENI, CONTROL NUMBER NA MPANGO WA UBORESHAJI STENDI NDOGO
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, katika ukumbi wa Jiji la Arusha, wakati akizungumza na waandishi wa habari, wakiwemo watumishi wa jiji hilo, kufuatia madai yaliyoibuliwa kupitia vyombo vya habari kuhusu ucheleweshaji wa control number, kuondolewa kwa wafanyabiashara kwenye vibanda na madai ya kunyanyaswa kwa wazawa.
Akizungumza kwa msisitizo, Mkude alisema madai hayo hayana ukweli, na yanapotosha umma kuhusu juhudi za serikali katika kusimamia haki, usawa na maendeleo ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa ndani ya jiji hilo.
KIKAO RASMI CHA WAFAANYABIASHARA
Alieleza kuwa tarehe 22 Januari 2024, halmashauri ya jiji ilifanya kikao rasmi kilichowakutanisha viongozi wa wafanyabiashara wa mji, viongozi wa mitaa na vijiji pamoja na uongozi wa halmashauri, kwa lengo la kujadili kwa kina madeni ya wafanyabiashara yanayodaiwa na serikali ya jiji.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa katika kikao hicho, jumla ya madeni yanayodaiwa yanafikia takribani shilingi bilioni 1.7, huku sehemu kubwa ya madeni hayo ikitokana na wafanyabiashara wachache waliokiuka ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali kwa muda mrefu.
Alibainisha kuwa mfanyabiashara aliyetoa malalamiko, Dominic Mwele, ni miongoni mwa wanaodaiwa, na kwa zaidi ya miaka mitatu amekuwa akiendesha shughuli zake bila kutimiza ipasavyo masharti ya mikataba na ulipaji wa stahiki zake.
MADENI NI MSINGI WA HUDUMA ZA MAENDELEO
Mkude alisema ukusanyaji wa mapato ya ndani si adhabu kwa wafanyabiashara, bali ni msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Mapato hayo yanatumika kugharamia:
Ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya
Ununuzi wa vifaa tiba na mashine za kisasa
Ajira ya madaktari, wauguzi na watumishi wa afya
Ukarabati wa barabara za TARURA na barabara za ndani ya jiji
Uboreshaji wa masoko ya Mrombo na Kilombero
Ujenzi na ukarabati wa vyoo na miundombinu ya masoko
Ununuzi wa magari ya usafi wa mazingira na ukusanyaji wa taka
STENDI NDOGO: UBORESHAJI NI MPANGO RASMI
Akizungumzia eneo la Stendi Ndogo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema hakuna mfanyabiashara anayepaswa kuondolewa kiholela, akisisitiza kuwa taratibu za kuhamisha wafanyabiashara zinafahamika kisheria na zitazingatiwa kikamilifu.
Alisema uboreshaji wa Stendi Ndogo ni mpango rasmi wa serikali wa muda mfupi, uliomo kwenye maandalizi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025, na hautavuruga shughuli za kawaida za wafanyabiashara.
“Serikali itahakikisha wafanyabiashara wanahamishwa kwa utaratibu kwenda maeneo mbadala wakati wa uboreshaji na kurejeshwa mara baada ya mradi kukamilika,” alisema Mkude.
MALALAMIKO YA MTU BINAFSI
Mkude alisema wazi kuwa malalamiko hayo hayawakilishi wafanyabiashara wote, bali ni ya mtu binafsi mwenye maslahi yake, akieleza kuwa serikali imefanikiwa kupata nakala halisi za mikataba ya maeneo husika kuanzia mwaka 1993 kutoka katika hifadhi za nyaraka za serikali.
SERIKALI YATOA ONYO
Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwa serikali haitavumilia upotoshaji, uchochezi wala matumizi mabaya ya vyombo vya habari kwa maslahi binafsi, akiongeza kuwa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia haki, uwazi na usawa kwa wananchi wote bila ubaguzi.


0 Comments