MGOGORO WA FEDHA WATINGISHA EAC,RAIS RUTO AITISHA MKUTANO WA DHARURA ARUSHA,DENI LAFIKIA DOLA MIL.89,DRC ILIONGOZA KUDAIWA DOLA MIL.27.

Mgogoro wa Fedha Watingisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); William Ruto Aita Mkutano wa Dharura Arusha

By Arushadigital 


RAIS wa Kenya, William Ruto, ameita mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Machi 7, 2026 jijini Arusha, katika hatua inayolenga kukabiliana na mgogoro mkubwa wa kifedha unaotikisa uhai na ufanisi wa jumuiya hiyo ya kikanda.

Mkutano huo, unaotarajiwa kuwa wa kwanza kufanyika baada ya zaidi ya mwaka mmoja, unakuja wakati EAC ikikabiliwa na pengo kubwa la fedha linalotishia utekelezaji wa mipango yake ya kimkakati, ikiwemo miradi ya ushirikiano wa kiuchumi, biashara ya kikanda na mageuzi ya huduma za umma. 


Viongozi hao wanatarajiwa kujadili mfumo mpya wa uchangiaji wa fedha pamoja na hatua kali za kudhibiti matumizi, kufuatia nchi wanachama kushindwa kuwasilisha zaidi ya dola za Marekani milioni 89.3 zinazodaiwa na taasisi za jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, hadi Januari 31, 2026, EAC ilikuwa inaidai nchi wanachama dola 89,372,865. Takwimu zinaonyesha kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaongoza kwa deni la takribani dola milioni 27, ikifuatiwa na Burundi (dola milioni 22.7), Sudan Kusini (dola milioni 21.8), Somalia (dola milioni 10.5), Rwanda (dola milioni 5.2) na Uganda (dola milioni 1.1). Tanzania pamoja na Kenya ndizo pekee zilizokuwa zimelipa kikamilifu mchango wa dola milioni saba kwa mwaka wa fedha 2025/26.



Ruto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi wa EAC, anatarajia marais wote wanane wa nchi wanachama kushiriki, akisisitiza kuwa mustakabali wa kifedha wa jumuiya hiyo uko mikononi mwa viongozi hao wakuu. Hatua ya kuitisha mkutano wa dharura inaonekana kama jaribio la kuirejesha EAC katika mwelekeo thabiti wa kiutendaji na kuimarisha nidhamu ya kifedha miongoni mwa wanachama.

Waziri wa Kenya anayeshughulikia Masuala ya EAC, Mikoa Kame na Maendeleo ya Kanda, Beatrice Askul, amesema mkutano huo utatoa majibu ya kisera kuhusu uhaba wa fedha unaoikabili jumuiya hiyo, ikiwa ni pamoja na kupitishwa kwa mfumo mpya wa ufadhili uliopendekezwa na Baraza la Mawaziri la EAC na kuafikiwa kwa mwongozo wa pamoja wa matumizi.

“Rais wa Kenya ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano wa wakuu wa nchi ana nia ya dhati kuona viongozi wanatoa msimamo wao kuhusu suala hili, kwa sababu wao ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi ndani ya EAC,” amesema Askul.

Mgogoro huo wa kifedha tayari umeanza kuathiri uendeshaji wa taasisi muhimu za kikanda, zikiwamo Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), pamoja na programu nyingine za ushirikiano wa kikanda zinazolenga kuimarisha biashara, uwekezaji na uhuru wa usafirishaji ndani ya Afrika Mashariki.

Wachambuzi wa masuala ya kikanda wanaona mkutano huo wa Arusha kuwa kipimo muhimu cha mshikamano wa kisiasa na kiuchumi ndani ya EAC, huku wakionya kuwa kuchelewa kupata suluhisho la kudumu kunaweza kudhoofisha kasi ya utekelezaji wa ajenda ya soko la pamoja na malengo ya ujumuishaji wa kikanda.

Hatima ya mfumo mpya wa uchangiaji wa fedha na mkakati wa kurejesha uthabiti wa kifedha wa EAC sasa inasubiri maamuzi ya wakuu wa nchi, katika mkutano unaotarajiwa kuwa na athari pana kwa mustakabali wa ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Ends..

Post a Comment

0 Comments