MAKAME WMA YANG’ARA SERENGETI AWARDS, SERIKALI YATAMBUA JUHUDI ZA JAMII KATIKA UHIFADHI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame (WMA) kutoka Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, imeendelea kujijengea heshima katika sekta ya uhifadhi baada ya kunyakua tuzo ya The Serengeti Awards, tuzo inayotolewa na Serikali kwa taasisi na wadau waliotoa mchango mkubwa katika kulinda rasilimali za wanyamapori, misitu na mazingira kwa ujumla.
Tuzo hiyo, iliyotolewa usiku wa kuamkia leo katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, inaashiria utambuzi rasmi wa jitihada za jamii ya Makame katika kutekeleza uhifadhi shirikishi unaolenga kulinda mazingira huku wananchi wakinufaika kiuchumi na kijamii.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo leo Januanri 31,2026, Katibu wa Makame WMA alisema ushindi huo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na wananchi kwa kushirikiana na Serikali katika kusimamia rasilimali za asili kwa uwajibikaji na uzalendo wa hali ya juu.
Alieleza kuwa Makame WMA imekuwa mfano bora wa maeneo ya hifadhi yanayosimamiwa na jamii, ambapo mshikamano kati ya viongozi wa Serikali za mitaa, viongozi wa vijiji, watumishi wa WMA na mashirika yasiyo ya kiserikali umechangia mafanikio makubwa katika uhifadhi endelevu.
Katibu huyo alibainisha kuwa juhudi hizo zimewezesha kupungua kwa vitendo vya ujangili, kuimarika kwa ulinzi wa misitu na kupunguzwa kwa migogoro kati ya binadamu, mifugo na wanyamapori kupitia utekelezaji wa mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi.
Aliongeza kuwa tuzo hiyo ni chachu mpya ya kuongeza nidhamu ya kazi, uwajibikaji na ubunifu katika kusimamia Makame WMA, huku akisisitiza kuwa jamii itaendelea kushirikishwa kikamilifu ili kuhakikisha uhifadhi unaleta tija ya moja kwa moja kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya maeneo ya WMA.
Hafla ya utoaji wa tuzo za Serengeti Awards ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa uhifadhi pamoja na sekta binafsi, huku Mgeni Rasmi akiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwisho.



0 Comments