SHAYONA SAFARIS YASHUKURU KUTEULIWA TUZO YA “BEST DOMESTIC TOUR OPERATOR” – SERENGETI AWARDS,YAPOKEA TUZO NZITO

 SHAYONA SAFARIS YASHUKURU KUTEULIWA TUZO YA “BEST DOMESTIC TOUR OPERATOR” – SERENGETI AWARDS

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA



ARUSHA: Kampuni ya utalii ya Shayona Safaris and Tours Ltd imeeleza shukrani zake za dhati baada ya kuteuliwa kushindania tuzo ya Best Domestic Tour Operator Award katika hafla ya Serengeti Awards, tukio lililofanyika usiku wa kuamkia Januari 31, 2026 katika Hoteli ya Mt Meru, Arusha.


Hafla hiyo ilihudhuriwa na watoa huduma mbalimbali wa sekta ya utalii, wamiliki wa hoteli, mashirika ya ndege, pamoja na wadau wa serikali na binafsi walioko mstari wa mbele katika kukuza utalii wa Tanzania.Mgeni rasmi katika tuzo hizo alikuwa ni Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba


Akizungumza kwa niaba ya timu nzima ya kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Shayona Safaris and Tours Ltd, Nisha Karelia, alisema uteuzi huo ni heshima kubwa na uthibitisho wa kazi nzuri, juhudi na kujituma kwa wafanyakazi wake katika kuitangaza Tanzania kama kivutio cha kimataifa.


“Awali ya yote, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka na ulinzi wake katika safari yetu yote. Bila neema zake, mafanikio haya yasingewezekana,” alisema Karelia, akiendelea:

“Pia tunawashukuru wateja wetu waaminifu, ambao kwa imani na ushirikiano wao wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yetu. Bila wateja wetu, safari hii ya mafanikio haingekuwa halisi.”Alisema.


Aidha, Mkurugenzi huyo aliongeza shukrani za pekee kwa familia ya Shayona, akisisitiza kuwa imani, ushirikiano na msaada wao wa muda mrefu umekuwa nguzo ya mafanikio ya kampuni. 


Pia alitaja wafanyakazi wote, hususan madereva waongozaji (tour guides), kwa bidii, uzalendo na kujituma kuhakikisha wageni wanapata huduma bora na uzoefu wa kipekee wa vivutio vya asili vya Tanzania.


“Kila mfanyakazi ameweka mchango wake kwa moyo na juhudi. Huu ni ushindi wa timu nzima,” aliongeza.


Mkurugenzi Karelia pia alishukuru Tuzo za Serengeti kwa kutambua mchango wa Shayona Safaris katika sekta ya utalii na kutoa wito kwa watendaji wa tuzo hizo kuendelea kuandaa hafla hii kila mwaka ili kuhamasisha ubora na ushindani katika sekta ya utalii nchini.


Akihitimisha, Karelia aliahidi kuwa Shayona Safaris and Tours Ltd itaendelea kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa, huku akiwataka wadau wote kushirikiana katika kulinda na kuitangaza Tanzania kama kivutio kisichosahaulika, huku akisisitiza kwamba Serengeti itaendelea kuishi milele.


“Tunatambua kuwa utalii ni urithi wa taifa letu. Ni wajibu wetu sote kuutunza, kuuhifadhi na kuutangaza vizazi vijavyo,” alisisitiza.


Hafla ya Serengeti Awards imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua juhudi za wadau wa utalii, kuhimiza ubora wa huduma, na kuendeleza ushindani mzuri katika sekta hiyo, huku ikithibitisha Tanzania kama moja ya malengo makuu ya utalii wa ndani na kimataifa.


Ends.


Post a Comment

0 Comments