TANAPA YAPOKEA TUZO ZA SERENGETI AWARDS KWA MAENDELEO YA UTALII

TANAPA YAPOKEA TUZO YA MAENDELEO YA UTALII KWA NIABA YA KOICA

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA 



KAMISHNA wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA Musa Nassoro Kuji, Januari 31, 2026 alipokea tuzo ya heshima ya “Best Development Partner Supporting Tourism Development” kwa niaba ya Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), katika hafla kubwa ya utoaji wa Tuzo za Serengeti Awards iliyofanyika katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abasi, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa KOICA katika kuendeleza sekta ya utalii na uhifadhi nchini, hususan kupitia ujenzi wa Kituo cha Serengeti Media Centre kilichopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, ilielezwa kuwa mradi wa Serengeti Media Centre umeleta mageuzi makubwa katika namna vivutio vya utalii na ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti vinavyotangazwa na kuwasilishwa kwa wageni. Kupitia teknolojia ya kisasa, kituo hicho kinawawezesha watalii kupata maudhui ya picha mjongeo na mnato yanayoonesha kwa undani uzuri wa hifadhi, maisha ya wanyamapori na mifumo ya ikolojia ya Serengeti.

Uanzishwaji wa kituo hicho umeelezwa kuwa chachu muhimu katika kuboresha uzoefu wa watalii, kuongeza uelewa wa masuala ya uhifadhi, pamoja na kuimarisha juhudi za TANAPA katika matumizi ya teknolojia ya kisasa kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Katika hatua nyingine, Kamishna wa TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji, pia alipata fursa ya kukabidhi tuzo ya kipengele cha “Best Conservation Influencer”, ambapo mshindi alikuwa ni Nakaaya Sumari, kwa mchango wake mkubwa katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na wanyamapori kupitia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano na ubunifu wa kijamii.

Tuzo za Serengeti Awards zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kitaifa na kimataifa katika kutambua mchango wa wadau wa sekta ya utalii na uhifadhi, zikiwemo taasisi, washirika wa maendeleo, wabunifu na watu binafsi waliotoa mchango wa kipekee. Kupitia tuzo hizo, Tanzania inaendelea kuimarisha hadhi yake kimataifa kama kinara wa utalii wa safari na uhifadhi wa wanyamapori barani Afrika na duniani kwa ujumla.







Ends..

Post a Comment

0 Comments