MAJAMBAZI 3 WAUAWA KWA RISASI BARIADI Polisi wanasa AK-47, fedha za kigeni; watuhumiwa wadaiwa kuvamia taasisi ya Fedha

MAJAMBAZI 3 WAUAWA KWA RISASI BARIADI

Polisi wanasa AK-47, fedha za kigeni; watuhumiwa wadaiwa kuvamia taasisi ya fedha

Na Arushadigital | SIMIYU



Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limewaua watu watatu wanaodaiwa kuwa majambazi kufuatia majibizano ya risasi na kikosi maalum cha polisi usiku wa kuamkia leo Februari 8, 2026, katika Wilaya ya Bariadi.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, operesheni hiyo ilifanyika baada ya kupokea taarifa za kiintelijensia kuwa watu hao walikuwa wakivunja milango ya jengo la Simiyu Money Services wakilenga kuiba fedha za miamala ya kibenki na simu.

Wahalifu hao walijeruhiwa vibaya wakati wa majibizano ya risasi na baadaye walifariki dunia wakiwa njiani kupelekwa hospitali kwa matibabu.

Katika eneo la tukio, polisi walikamata silaha moja aina ya AK-47 ikiwa na risasi nane. Upekuzi wa awali pia ulibaini kuwepo kwa fedha za kigeni zikiwemo shilingi 300 za Kenya na noti ya Misri, pamoja na tiketi za basi zinazoonyesha watuhumiwa walitokea Migori, Kenya kupitia Sirari hadi Lamadi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao wa kutoa taarifa zilizosaidia kuzuia tukio hilo la uhalifu mkubwa.

Aidha, polisi wametoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya kijinai, wakisisitiza kuwa operesheni na misako itaendelea ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa ipasavyo.

Ends..


Post a Comment

0 Comments