By Arushadigital
Mahakama Kuu ya Zambia, Kitengo cha makosa ya rushwa na Uhujumu Uchumi, imetaifisha mali za Dalitso Lungu, mtoto wa kiume wa aliyekuwa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Edgar Lungu. Hukumu hiyo imesomwa leo mjini Lusaka ambapo mali zilizotaifishwa ni magari 79, yakiwemo magari ya kifahari kama Rolls Royce, Mercedes-Benz, Ferrari na Lamborghini, ambayo amekuwa akionekana nayo katika maeneo ya kifahari mjini Lusaka na Afrika Kusini.
Pamoja na magari hayo, pia mahakama imetaifisha kituo kimoja cha mafuta mjini Lusaka kilichokuwa kinamilikiwa na Dalitso, pamoja na nyumba 6 za kifahari alizonunua maeneo ya Ibex Hill na Silverest (Lusaka), pamoja na mitaa ya kitajiri ya Riverside na Parklands huko Copperbelt. Amebakiziwa nyumba moja aliyopewa zawadi na baba yake.
Mahakama imesema imetaifisha mali hizo kwa kuwa Dalitso hakuwa na kazi yoyote ya kumuingizia kipato, zaidi ya kuwa mtoto wa Rais. Kwa kuwa alishindwa kueleza mahakama jinsi alivyopata mali hizo, mahakama imetafsiri kuwa mali hizo ni zao la uhalifu na hivyo kuzitaifisha kuwa mali za umma kwa mujibu wa Sheria ya Mapato Yatokanayo na Uhalifu (Proceeds of Crime Act, Zambia, Kifungu cha 31).
Awali, upande wa mashtaka ulidai kuwa Dalitso alitumia nafasi ya baba yake akiwa madarakani kujilimbikizia mali kinyume na utaratibu. Sehemu ya hukumu hiyo imesema "Mahakama imebaini kuwa Dalitso Lungu hakuwa na kazi wala chanzo chochote halali cha mapato kinachoweza kueleza umiliki wa mali hizo, na hivyo kuanzia leo mali zake zote zinahesabiwa kama mapato ya uhalifu na zinataifishwa.”
Nyumba ambayo Dalitso alipewa zawadi na baba yake, imeondolewa katika orodha ya mali zilizotaifishwa na Mahakama. Upande wa mashtaka umeeleza kuwa unafuatilia kwa karibu nyumba za Dalitso anazodaiwa kumiliki Afrika Kusini na Dubai ili nazo zitaifishwe.
Haya yanatokea takribani miezi 8 tangu Rais Edgar Lungu afariki dunia, na mwili wake bado haujazikwa kutokana na mvutano uliopo kati ya familia na serikali ya Zambia. Serikali inataka Rais huyo wa zamani azikwe Zambia kwa heshima zote za kitaifa, lakini familia imekataa na kutaka azikwe Afrika Kusini bila uwepo wa kiongozi yeyote wa serikali.
Ends..

0 Comments