DC MKUDE AAGIZA NIDHAMU, USAFI NA UHAKIKI WA WAFANYABIASHARA ARUSHA
Auvunja mgogoro Kilombero, awaondoa wafanyabiashara barabarani
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ametoa agizo kali la kurejesha nidhamu, usafi na utaratibu katika masoko ya jiji, akisisitiza kuwa msongamano wa wafanyabiashara hauwezi kuwa kisingizio cha kuvunja sheria wala kuziba miundombinu ya soko.
Akizungumza jana katika ukaguzi wa ghafla wa Soko Kuu la Arusha baada ya kupokea malalamiko ya kuzibwa kwa barabara za ndani, DC Mkude alisema Serikali haitavumilia biashara holela inayokwamisha upitishaji wa wananchi na kupunguza mapato ya jiji.
“Msongamano hauhalalishi kuziba barabara. Kila mfanyabiashara arejee kwenye eneo lake rasmi ili haki itendeke,” alisisitiza.
Alielekeza wafanyabiashara wote waliokuwa wakifanya biashara kwenye barabara za ndani kuondoka mara moja, huku akitangaza kuwa kuanzia Jumatatu ijayo zoezi la kuwarejesha kwa nguvu katika maeneo yao halali litaanza sambamba na uhakiki wa wafanyabiashara wote.
Katika hatua hiyo, Serikali itakusanya taarifa za wafanyabiashara halali na kudhibiti tabia ya kulipia meza kisha kuzikodisha au kuzitelekeza.
“Ukishalipia meza unatakiwa ufanye biashara mwenyewe. Upangishaji wa vizimba au meza hautakubalika,” alionya.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara wasiokuwa na maeneo maalumu kujisajili kwa viongozi wa soko ili kupangiwa sehemu rasmi, huku akisisitiza umuhimu wa usafi wa mazingira wakati Arusha ikijiandaa kupokea wageni wengi mwaka 2027 katika mashindano ya AFCON.
“Bidhaa za chakula ziwekwe juu ya meza, si chini. Usafi ni jukumu letu sote,” alisisitiza.
Katika ukaguzi huo, DC Mkude alibaini mama ntilie wanaofanya biashara kwenye korido na changamoto ya vyoo kukosa maji, na kuagiza mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kurejesha huduma.
Katika hatua nyingine, DC Mkude alivunja mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda katika Soko Namba 68 la Kilombero, akirejesha utaratibu kwa kuwaondoa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara kando ya barabara.
Alielekeza wafanyabiashara wote waliokuwa nje ya soko kuingia mara moja ndani ya eneo rasmi la biashara, akisema hakuna mfanyabiashara aliye juu ya sheria.
“Waliopo nje waondoke barabarani mara moja. Namuelekeza Mkurugenzi afungue mageti ili waingie ndani ya soko, na mkandarasi arudishe nyuma uzio wake wa mabati,” alisema huku akishangiliwa na wafanyabiashara.
Katika hatua ya mpito, mageti ya eneo la mradi wa soko la kisasa yalifunguliwa ili kuwapa nafasi ya muda wafanyabiashara wasiokuwa na maeneo maalumu wakati ujenzi ukiendelea.
Pia aliahidi wafanyabiashara waliopo ndani ya soko watapatiwa mikataba halali ya biashara na kuonya tabia ya kupangisha vizimba kwa wengine.
Kuhusu huduma za umeme, aliwataka wafanyabiashara kuomba mita binafsi za TANESCO ili kuondokana na mfumo wa muda unaosababisha usumbufu wa huduma.
Hatua za DC Mkude zimeelezwa kuwa pigo kwa biashara holela na hatua muhimu ya kuimarisha utaratibu, afya ya jamii na mapato ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
— MWISHO —



0 Comments