Na Joseph Ngilisho – Arusha
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameagiza uongozi wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI) kilichopo Njiro, Arusha, kuanza uzalishaji wa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARV) ifikapo mwezi Juni 2026.
Hatua hii inalenga kupunguza utegemezi wa nchi katika kuagiza dawa kutoka nje na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa tiba kwa wagonjwa.
Agizo hilo limekuwa sehemu ya ziara ya Waziri Mchengerwa katika kiwanda hicho Januari 27, 2026, ambacho kimesitisha uzalishaji wa dawa tangu mwaka 2013 kutokana na changamoto za kifedha na kiutawala.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Mchengerwa alisema kiwanda cha TPI kina uwezo mkubwa wa uzalishaji, ikiwa na uwezo wa kutengeneza zaidi ya tembe za dawa milioni 1.7 ndani ya saa 10, lakini kilishindwa kuendelea na uzalishaji kutokana na maslahi binafsi ya baadhi ya watu waliokosa uzalendo.
“Ni jambo lisilokubalika kwa kiwanda chenye uwezo mkubwa kama hiki kusimama kwa zaidi ya muongo mmoja kwa sababu ya watu wachache waliotanguliza maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya Taifa,” alisema Waziri.
Alibainisha kuwa Tanzania kwa sasa inaagiza dawa kutoka nje kwa zaidi ya asilimia 90, hali ambayo inahatarisha bajeti ya Serikali na kuchelewesha utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo katika sekta ya afya.
Kutokana na hali hiyo, Waziri aliagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuhakikisha Shilingi bilioni 20 zinatengwa mara moja kwa ajili ya maandalizi ya haraka ya kuanza uzalishaji wa dawa, hususan dawa za ARV, kabla ya Juni 2026.
“Ninamuagiza Katibu Mkuu atenge shilingi bilioni 20. Sitaki kuona mtu yeyote au taasisi yoyote ikijaribu kukwamisha mchakato huu. Atakayethubutu kufanya hivyo hatavumiliwa na atahesabika kama mpinga maendeleo,” alisisitiza.
Faida za uzalishaji wa ndani
Waziri Mchengerwa aliongeza kuwa uzalishaji wa dawa za ARV ndani ya nchi utasaidia kuimarisha usalama wa dawa, kupunguza gharama za ununuzi wa dawa kutoka nje, na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa tiba kwa wagonjwa wa UKIMWI nchini.
Kiwanda cha TPI kilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 kwa lengo la kuzalisha dawa muhimu kwa matumizi ya ndani. Kimefanyiwa maboresho makubwa mwaka 2013, lakini kilishindwa kuendelea na uzalishaji kwa zaidi ya muongo mmoja hadi Serikali ilipoingilia kati.
Hatua ya Serikali ya kufufua kiwanda hicho ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uzalishaji wa dawa ndani ya nchi na kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.
Mbunge wa Arumeru Magharibi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya, Dkt. Johannes Lukumay, aliwahakikishia Watanzania kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu, ikiwemo dawa za ARV, unaendelea bila kukwama licha ya changamoto za kimataifa za ufadhili wa sekta ya afya.
“Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali ipo imara. Tuna akiba ya dawa, tuna mipango mbadala, na tunaendelea kuimarisha uzalishaji wa dawa ndani ya nchi ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayekosa huduma muhimu za afya,” alisema Dkt. Lukumay.
Aliongeza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya inaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya pamoja na wadau wa sekta ya afya ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi, huku utegemezi wa wafadhili wa nje ukipunguzwa hatua kwa hatua.
Dkt. Lukumay aliitaka Serikali kutoa mara moja Shilingi bilioni 25 zilizopangwa kwa ajili ya kukamilisha maboresho ya kiwanda hicho, hatua itakayofanikisha kuanza uzalishaji wa dawa ifikapo Juni 2026.
“Naomba fedha hizi zitolewe mara moja ili kiwanda kianze uzalishaji kwa wakati na kuondoa kabisa hofu ya upungufu wa dawa nchini,” alisisitiza.
Dkt. Lukumay pia alipongeza juhudi za Wizara ya Afya, uongozi wa Mkoa wa Arusha pamoja na wataalamu wa afya kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda na kuboresha afya za Watanzania.
Aliwahimiza wananchi kuendelea kuwa watulivu, kuiamini Serikali yao, na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Ziara ya Waziri Mchengerwa katika kiwanda cha TPI ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhimiza uzalishaji wa dawa ndani ya nchi, hatua itakayosaidia kuimarisha usalama wa dawa, kupunguza gharama za uagizaji, na kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa wananchi kwa uhakika.
Ends..













0 Comments