POLISI WANAWAKE MANYARA WAHIMIZA UTALII WA NDANI TARANGIRE
Na Arushadigital – MANYARA
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Christina Mkonongo kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF–Net) mkoani humo, ameongoza ziara ya utalii wa ndani kwa askari wa kike na wakaguzi wa Polisi Wilaya ya Babati pamoja na vikosi mbalimbali vya Polisi Mkoa wa Manyara, kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Katika ziara hiyo, SSP Mkonongo aliambatana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Babati (OCD), Mrakibu wa Polisi (SP) Ernesta Mwambinga. Lengo la ziara hiyo lilikuwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha utalii wa ndani, sambamba na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, SSP Mkonongo alisema kuwa taasisi za umma, ikiwemo Jeshi la Polisi, zina wajibu wa kuwa mfano kwa vitendo katika kuhamasisha utalii wa ndani, kwani sekta hiyo ni mhimili muhimu wa uchumi na chanzo cha ajira kwa wananchi wengi.
Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ipo kaskazini mwa Tanzania, mkoani Manyara, kando ya barabara ya Arusha–Babati. Hifadhi hiyo inajulikana kwa makundi makubwa ya tembo, miti mikubwa ya mibuyu (baobab) pamoja na Mto Tarangire, ambao huvutia wanyama wengi hasa kipindi cha kiangazi, na kuifanya kuwa moja ya vivutio vikubwa vya utalii nchini.
Ends..
















0 Comments