POLISI MANYARA YAWATAKA WAZAZI KUIMARISHA ULINZI WA WATOTO KATIKA VITUO VYA MABASI
Na ArushaDigital – Babati, Manyara
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Manyara limewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa waangalifu zaidi kwa watoto wao wanapokuwa katika vituo vya kusubiria mabasi na stendi za daladala, ili kulinda usalama, malezi na maadili ya watoto hao.
Wito huo umetolewa Januari 23, 2026 na Sajenti wa Polisi Dotto Aloyce kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani Polisi Wilaya ya Babati, Dawati la Elimu, wakati akitoa elimu ya nafasi na wajibu wa mzazi katika vituo vya mabasi kwa abiria waliokuwa wakisubiri usafiri mjini Babati mkoani Manyara.
Akiwaelimisha wazazi na walezi waliokuwa na watoto wao, Sajenti Dotto alisema ni muhimu kwa wazazi kuwa karibu na watoto muda wote wanapokuwa stendi au vituo vya mabasi, badala ya kuwaacha wakizurura au kuvuka barabara bila uangalizi, jambo ambalo linaweza kusababisha ajali na madhara makubwa.
Alisisitiza kuwa vituo vya mabasi na stendi huwa na mikusanyiko mikubwa ya watu pamoja na shughuli mbalimbali, hali inayoongeza hatari kwa watoto endapo hawatasimamiwa ipasavyo, hivyo elimu ya usalama wa mtoto barabarani ni ya lazima kwa kila mzazi na mlezi.
Jeshi la Polisi limekumbusha jamii kuendelea kuchukua tahadhari wanaposafiri na watoto au wanapokuwa katika stendi na vituo vya mabasi wakisubiri usafiri, ili kuhakikisha usalama wa watoto hao unalindwa na kuzuia matukio ya ajali yanayoweza kuepukika.
Ends..


0 Comments