MCHENGERWA AMPA TANO DKT. LUKUMAY, ARIDHISHWA NA HUDUMA ZA HOSPITALI YA WILAYA OLTURUMENTI

MCHENGERWA AMPA TANO DKT. LUKUMAY, ARIDHISHWA NA HUDUMA ZA HOSPITALI YA WILAYA OLTURUMENTI

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amepongeza uongozi na wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi kwa kumchagua Mbunge makini na mwenye uwezo mkubwa wa kiuongozi, Dkt. Johannes Lukumay, akisema uamuzi huo umeleta matokeo chanya katika usimamizi wa sekta ya afya.

Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo januari 27,2026  baada ya kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Olturumenti iliyopo katika Halmashauri ya Arusha dc, mkoani Arusha, akiwa pamoja na Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Lukumay, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya.

Akizungumza na wananchi, watumishi wa afya na viongozi wa eneo hilo, Waziri Mchengerwa amesema Dkt. Lukumay ni kiongozi wa mfano ambaye ameonesha uwezo mkubwa tangu achaguliwe kuwa Mbunge na baadaye kuaminiwa na wabunge wenzake kuongoza kamati nyeti ya Bunge inayosimamia masuala ya afya, ikiwemo afya ya jamii, mapambano dhidi ya UKIMWI na masuala mengine muhimu ya ustawi wa Watanzania.

“Hongera nyingi sana kwa kazi kubwa mliyofanya ya kumchagua Dkt. Lukumay. Mlipoamua kumchagua kama Mbunge mlifanya uamuzi sahihi, lakini alipofika Bungeni ndipo tukagundua uwezo wake mkubwa zaidi,” alisema Mchengerwa.

Aliongeza kuwa kuchaguliwa kwa Dkt. Lukumay kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya ni ushahidi wa wazi wa imani kubwa aliyojijengea miongoni mwa wabunge, kutokana na weledi, unyenyekevu na uzalendo wake wa dhati.

Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa Dkt. Lukumay ni kiongozi anayejali maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla, akibainisha kuwa kila anapozungumza ndani na nje ya Bunge, hulenga kulinda afya za Watanzania na kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa hadi kuwafikia wananchi wote, hususan makundi maalum kama watoto, wajawazito, wazee na wananchi wenye mazingira magumu.

“Kila neno analolizungumza Dkt. Lukumay linaihusu nchi, linawahusu Watanzania na linagusa maisha ya watu. Ameendelea kuwasemea wananchi wa Arumeru na Watanzania kwa ujumla kwa ujasiri mkubwa,” amesisitiza Waziri huyo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mchengerwa amesema ameridhishwa na hali ya utoaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Olturumenti, huku akiahidi kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana kwa karibu na Mbunge huyo pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Arumeru ili kuimarisha zaidi miundombinu, vifaa tiba na rasilimali watu katika hospitali hiyo.

“Kwa nafasi yangu kama Waziri wa Afya, nitaendelea kufanya kazi kwa karibu na Dkt. Lukumay kuhakikisha sekta ya afya inalindwa na kuimarishwa kwa maslahi ya Watanzania wote,” amesema.

Alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi wa Arumeru kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao na kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya na maendeleo ya kijamii kwa ujumla na ikiwezekana Mwala 2030 aendelee kuwaomgoza.

Ends

Post a Comment

0 Comments