Dk LUKUMAY AINISHA CHANGAMOTO ZA AFYA ARUMERU MAGHARIBI, ATAKA HOSPITALI YA OLTRUMENT IPEWE KIPAUMBELE
Na Joseph Ngilisho – ARUMERU
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amezitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya katika jimbo lake, akimueleza Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, kuwa pamoja na uwekezaji mkubwa wa Serikali, bado kuna vikwazo vinavyokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza leo januari 27 ,2026 wakati wa ziara ya Waziri Mchengerwa katika hospitali ya Oltrument jimboni humo, Dkt. Lukumay alianza kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni tisa katika sekta ya afya nchini.
Alisema uwekezaji huo umejikita katika ununuzi wa vifaa tiba, utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya afya pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya.
“Jambo kubwa na la kupongezwa sana ni uamuzi wa Mheshimiwa Rais kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati wote. Kwa sasa wananchi wengi wanapata huduma za matibabu bila changamoto ya upungufu wa dawa, hali iliyopunguza mateso na gharama kwa wananchi,” alisema Dkt. Lukumay.
Hata hivyo, Mbunge huyo alisema bado kuna changamoto kadhaa zinazohitaji ufumbuzi wa haraka ili uwekezaji unaofanywa uwe na tija kwa wananchi wa Arumeru Magharibi.
Changamoto ya Maji Hospitalini
Dkt. Lukumay alieleza kuwa upatikanaji wa maji katika hospitali ya Oltrument na vituo vingine vya afya ni changamoto kubwa, akisisitiza kuwa huduma za afya haziwezi kutolewa kwa ufanisi bila maji ya uhakika.
“Hospitali bila maji ni sawa na jengo tupu. Tunaomba wizara isaidie kuweka utaratibu wa kudumu wa upatikanaji wa maji ili huduma zitolewe kwa viwango vinavyostahili,” alisema.
Hospitali Bila Uzio
Aidha, alibainisha kuwa hospitali ya Wilaya ya Arumeru Magharibi haina uzio wa uhakika, hali inayohatarisha usalama wa wagonjwa, watumishi na mali za Serikali.
“Eneo lote la hospitali liko wazi. Hii si salama. Tunaomba hospitali ipatiwe uzio ili kuimarisha usalama na mazingira ya utoaji wa huduma,” alisisitiza.
Uhaba wa Watumishi wa Afya
Katika hatua nyingine, Dkt. Lukumay alizungumzia tatizo la upungufu wa watumishi wa afya, akieleza kuwa licha ya uwekezaji mkubwa wa miundombinu, bado vituo vingi vina wahudumu wachache kupita kiasi.
Alisema katika baadhi ya vituo, mganga mmoja hulazimika kuhudumia wagonjwa wote, hali inayosababisha mzigo mkubwa kwa watumishi na kushusha ubora wa huduma.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, kuna haja ya kuongezewa wataalam wa kada mbalimbali ikiwemo,Wataalam wa dawa,Wataalam wa maabara,Wataalam wa fiziotherapia Na kada nyingine muhimu za afya.
Alisema kuongezwa kwa wataalam hao kutapunguza mzigo kwa waganga waliopo na kuboresha huduma kwa wananchi, hususan katika vituo vya afya vya ngazi ya msingi.
Akihitimisha, Dkt. Lukumay alimshukuru Waziri Mchengerwa kwa kutembelea hospitali hiyo, akisema uwepo wake ni ishara ya matumaini mapya kwa wananchi wa Arumeru Magharibi.
“Tunakupongeza Mheshimiwa Waziri kwa dhamira yako ya dhati ya kuboresha sekta ya afya. Uwepo wako hapa ni faraja kubwa kwa wananchi wetu,” alisema.





0 Comments