AJALI YA BASI NA LORI YATIKISA TINDE – SHINYANGA, UOKOAJI WAENDELEA

AJALI YA BASI NA LORI YATIKISA TINDE – SHINYANGA, UOKOAJI WAENDELEA

Na Joseph Ngilisho – ArushaDigital, SHINYANGA


Ajali mbaya ya barabarani imetokea asubuhi ya leo Januari 27, 2026, majira ya saa 12:00 asubuhi, katika eneo la Mnadani, Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, ikihusisha basi la abiria na lori la mizigo.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, ajali hiyo imehusisha basi la abiria la Kampuni ya KISILE lenye namba za usajili T 229 EEL, lililokuwa likifanya safari kutoka Kahama kuelekea Mwanza, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa likisafirisha shehena ya mchele kutoka Dar es Salaam kwenda nchini Rwanda.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa ajali hiyo ilitokea ghafla, hali iliyosababisha taharuki kubwa kwa wananchi wa eneo hilo pamoja na wasafiri waliokuwa wakipita barabara hiyo kwa wakati huo. Baadhi ya wananchi walijitokeza kutoa msaada wa awali kabla ya kuwasili kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na huduma za dharura.

Hadi sasa, juhudi za uokoaji zinaendelea, huku majeruhi wakikimbizwa katika vituo vya afya vilivyopo karibu kwa ajili ya kupata matibabu. Idadi kamili ya majeruhi au vifo bado haijathibitishwa rasmi.

Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama vipo eneo la tukio na vinaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo, huku madereva wakihimizwa kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan katika barabara zenye msongamano mkubwa .

Ends..

Post a Comment

0 Comments