LUKUMAY ATOA UHAKIKA UPATIKANAJI WA DAWA ZA ARV, AIPONGEZA SERIKALI KUFUFUA KIWANDA CHA KUZALISHA DAWA ARUSHA

LUKUMAY ATOA UHAKIKA UPATIKANAJI WA DAWA ZA ARV, AIPONGEZA SERIKALI KUFUFUA KIWANDA CHA KUZALISHA  DAWA ARUSHA,

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

MBUNGE wa Arumeru Magharibi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya, Dkt. Johannes Lukumay, amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu, ikiwemo dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARV), unaendelea bila kukwama licha ya changamoto za kimataifa za ufadhili wa sekta ya afya.

Dkt. Lukumay ametoa kauli hiyo leo jijini Arusha mara baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza dawa cha Njiro, akiwa pamoja na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, katika ziara maalum ya kukagua uwezo wa uzalishaji wa dawa nchini na kujionea jitihada za Serikali kufufua kiwanda hicho kilichosimama kwa takribani miaka 14.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Dkt. Lukumay alisema Serikali imepokea kwa uzito mkubwa wasiwasi wa wananchi, hususan wanaoishi na magonjwa sugu, kufuatia tetesi za uwezekano wa upungufu wa dawa za ARV kutokana na kusitishwa au kupungua kwa misaada ya nje, ikiwemo mpango wa PEPFAR.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali ipo imara. Tuna akiba ya dawa, tuna mipango mbadala, na tunaendelea kuimarisha uzalishaji wa dawa ndani ya nchi ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayekosa huduma muhimu za afya,” alisema Dkt. Lukumay.

Alieleza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya inaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya pamoja na wadau wa sekta ya afya ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi, huku utegemezi wa wafadhili wa nje ukipunguzwa hatua kwa hatua kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa alisema ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhimiza uzalishaji wa dawa ndani ya nchi, hatua itakayosaidia kuimarisha usalama wa dawa, kupunguza gharama za uagizaji na kuhakikisha upatikanaji wa uhakika kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Lukumay aliitaka Serikali kutoa kwa wakati fedha shilingi bilioni 25 zilizopangwa kwa ajili ya kukamilisha maboresho ya kiwanda hicho, ili kufanikisha azma ya kuanza uzalishaji wa dawa ifikapo Juni mwaka huu kama ilivyoelekezwa na Waziri wa Afya.

“Naomba fedha hizi zitolewe mara moja ili kiwanda kianze uzalishaji kwa wakati na kuondoa kabisa hofu ya upungufu wa dawa nchini,” alisisitiza.

Dkt. Lukumay pia amepongeza juhudi za Wizara ya Afya, uongozi wa Mkoa wa Arusha pamoja na wataalamu wa afya kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda na kuboresha afya za Watanzania.

Aliwahimiza wananchi kuendelea kuwa watulivu, kuiamini Serikali yao na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, akisisitiza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kulinda maisha ya wananchi wake.

Alihitimisha kwa kutoa shukrani kwa wananchi kwa imani yao kwa Serikali na kuwataka wadau wote wa sekta ya afya kuendelea kushirikiana katika kujenga mfumo imara wa afya unaojitegemea.






MWISHO


Post a Comment

0 Comments