Serikali Yaelekeza VETA Kupanuwa Wigo wa Wakufunzi wa Ukarimu na Utalii
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha elimu ya ufundi stadi kama mkakati wa makusudi wa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, ushindani wa kimataifa na mchango wa moja kwa moja katika uchumi wa taifa, huku Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kikitambuliwa kama mhimili muhimu katika kuandaa rasilimali watu kwa sekta nyeti za ukarimu na utalii zinazochangia kwa kiwango kikubwa pato la taifa.
Akizungumza leo Januari 05, 2026 alipokagua uendeshaji wa mafunzo ya amali yanayotolewa katika Chuo cha VETA cha Mafunzo ya Hoteli na Utalii Njiro, jijini Arusha, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ameir, alisema mafunzo hayo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, zinazolenga kujenga jamii iliyoelimika, yenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kikanda na kimataifa.
Ameir alisema chuo hicho kimekuwa mfano wa kuigwa kwa kuendesha mafunzo ya ukarimu na utalii yenye viwango vya juu, yanayojikita zaidi katika kujenga ujuzi wa vitendo unaowawezesha wahitimu kuajirika au kujiajiri mara baada ya kumaliza masomo yao.
Alisema kuwa uwepo wa hoteli ya mafunzo inayomilikiwa na chuo hicho ni ubunifu unaosaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo, huku pia ikiongeza mapato ya ndani ya chuo na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali, jambo linaloendana na dira ya uendelevu wa taasisi za elimu ya ufundi.
Aidha, Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo yameweka msisitizo mkubwa katika elimu ya ujuzi kuanzia ngazi ya msingi, na hivyo kuitaka VETA kupanua wigo wa kuandaa wakufunzi na walimu tarajali wa mafunzo ya amali, hususan katika fani za ukarimu na utalii, ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi nchini.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa rasilimali, vifaa vya kisasa na kuajiri wakufunzi wenye mbinu bora za ufundishaji, huku akiitaka VETA kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta binafsi katika ukarimu na utalii kwa lengo la kuongeza fursa za ajira, kukuza ujuzi unaoendana na soko la kazi, na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.
Ameir amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa utoaji wa mafunzo ya ufundi na ufundi stadi, kama nguzo muhimu ya kufanikisha azma ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda na kufikia hadhi ya uchumi wa kati unaojitegemea.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Arusha ,DC Joseph Mkude amesema Serikali inaendelea kuhamasisha vijana kujiunga na chuo cha veta Kwa kuwa ni kiunganishi Kikubwa cha utalii katika Kanda ya kaskazini.
Akitoa taarifa ya chuo, Mkuu wa chuo cha Veta cha mafunzo ya hoteli na utalii Njiro, Magubi Mabelele amesema chuo hicho kilianzishwa rasmi 2010 na 2013 kupata ithibati kutoka mamlaka ya usajili ya Nactivet.
Amesema hoteli iliyoko chuoni hapo imekuwa ikiingiza mapato ambayo yamekuwa yakitumika katika uendeshaji wa gharama za chuo pale ambapo makao makuu inapokuwa imezidiwa.
Aidha amesema chuo hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mabweni ya kulala wanafunzi jambo ambalo linawafanya kubuni namna ya kuweza kupokea wanafunzi wote kwa pamoja.
“ Chuo kina uwezo wa kudahili wanachuo 1200 kwa mwaka, kupitia fani tano za usafiri wa utalii, mapokezi, uokaji, upishi na usafi, pia tumekuwa tukitoa udahili kwa wanaotaka mafunzo mafupi pamoja na mafunzo maalum, hata hivyo tunachangamoto ya mabweni,” amesema.
Awali mkurugenzi wa Veta Kanda ya kaskazini Monica Mbele alisema ofisi yake inaendelea na ujenzi wa vyuo nane katika maeneo ya Wilaya katika Miko ya Kanda ya kaskazini ambayo hayakuwa na vyuo hivyo.
Alisema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyuo hivyo, Veta Kanda ya kaskazini itakuwa na jumla ya vyuo 22 na kuongeza idadi kubwa ya wahitimu.
Aidha alisema vyuo hivyo vina changamoto ya walimu kwa fani mbalimbali ikiwemo lugha, vifaa ikiwemo magari kwaajili ya waongoza watalii, kutokuwa na karakana ya fani ya utalii, upungufu wa hosteli na kulazimu vijana wengi kupanga mtaani,
Mkurugenzi wa VETA CPA Anthony Kasore alisema veta ina vyuo 80 katika Wilaya na Mikoa mbalimbali nchini, na vingine vimeendelea kujengwa.
Alisema VETA imeendelea kuongeza wigo wa ushirikiano na wadau wa nje ambao wamekuwa wakileta wanafunzi na kuwalipia Moja Kwa Moja kupitia kampuni zao ambapo Kwa Veta Arusha inapokea wanafunzi 80 wa Moja Kwa Moja kutoka Kwa wadau hao.
Alisema Hadi kufikia 2028 veta inataka kuwa na watumishi 4148 na hivi sasa wako watumishi 2100 na kuishukuru Serikali kuzipatia kibali cha kuajiri watumishi 500 ambapo kati yake wakifunzi ni asilimia70.
“ Mwaka huu tumepokea maombi ya wanafunzi jumla 18,000 na uwezo Wetu ni kuchukua wanafunzi 14000 lakini tumelazimika kuchukua wanafunzi wote., hata hivyo Vijana 1000 wataanza masomo ya jioni Ili kuwezesha wote wasome,”alisema.
Mkurugenzi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia mafunzo na ubunifu , Prof Fredrick Salukele amesema lengo la chuo hiki cha utalii ni kuongeza mapato na kupunguza utegemezi wa Wizara.
Ends..












0 Comments