WAZIRI WA FEDHA AAGIZA TRA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI NA KUONGEZA UWIANO WA MAKUSANYO

Waziri wa Fedha Aagiza TRA Kuimarisha Utendaji na Kuongeza Uwiano wa Makusanyo

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesisitiza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapaswa kuendeleza utendaji wake kwa kiwango cha juu zaidi, kuongeza uwiano wa ukusanyaji wa mapato, na kuhakikisha mifumo mipya ya ukusanyaji kodi inatumika kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia walipakodi.


 Akifungua Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Waziri Khamis aliagiza TRA kuendelea kupanua wigo wa walipakodi, hususan katika sekta zisizo rasmi, biashara mtandaoni, na uchumi wa kidijitali, huku akisisitiza mbinu rafiki na zenye kuzingatia utu wa mlipakodi ili kujenga uhusiano thabiti wa kuaminiana.

Aidha, Waziri aliongeza kuwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni matokeo ya jitihada za pamoja na sera madhubuti za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. 


Katika sehemu ya pongezi, Balozi Khamis aliwapongeza viongozi na watumishi wa TRA kwa kuonesha ufanisi mkubwa katika ukusanyaji wa mapato; katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, TRA ilikusanya shilingi trilioni 18.77, sawa na asilimia 103.7 ya lengo la trilioni 18.10 lililowekwa.


“Mwezi Desemba pekee, mmeweka rekodi mpya kwa kukusanya shilingi trilioni 4.13 – kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hii. Mafanikio haya ni kiashiria thabiti kwamba TRA ipo katika mwelekeo mzuri wa kufanikisha na hata kuvuka lengo la mapato lililopangwa kwa mwaka wa fedha 2025/26. Hongereni sana kwa jitihada zenu,” alisema Balozi Khamis, akisisitiza kwamba jitihada hizi zinapaswa kuendelezwa kwa kasi endelevu.


Waziri huyo alibainisha kuwa mafanikio haya yanatokana na uwekezaji makini katika mifumo ya ukusanyaji wa mapato, mageuzi ya sera za kodi, na matumizi ya teknolojia za kisasa, hatua ambazo zimeleta mapinduzi makubwa katika ukusanyaji wa mapato na kuongeza uwiano wake.


 Alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) unafanya kazi kikamilifu mara tu baada ya kuzinduliwa rasmi, ili kuongeza uwazi, ufanisi na udhibiti wa mapato.

Naibu Mawaziri wa Fedha,  Mhandisi Mshamu Ali Munde na Laurent Luswetula, wameahidi kushirikiana kwa karibu na Waziri ili kuhakikisha TRA inaendelea kutimiza malengo yake ya muda mfupi na mrefu, huku ikiboresha zaidi uhusiano wake na walipakodi na kuhakikisha malengo ya maendeleo ya Serikali yanafanikiwa.


Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRA, Dkt. Albina Chuwa, alisema kuwa Mamlaka itaendelea kupanua wigo wa walipakodi kutoka milioni 7 hadi milioni 21, hatua itakayoongeza mapato kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga mfumo wa makusanyo unaoendelea kushirikisha jamii nzima.


Kamishna wa TRA, Yusuph Mwenda, aliwapongeza wafanyabiashara kwa utaratibu wao wa kulipa kodi kwa hiari, jambo lililosaidia kufanikisha malengo ya Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26. Aliongeza kuwa TRA imepata ukuaji chanya wa asilimia 13.6 katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, ishara yenye nguvu kwamba jitihada za Serikali na Mamlaka zinakidhi matokeo chanya katika kusimamia mapato ya Serikali.


“Ufanisi huu ni kiashiria thabiti kwamba lengo la makusanyo ya Shilingi trilioni 36.06 kwa mwaka wa fedha 2025/26 linaweza kufanikishwa kikamilifu.


 "Tumeweka malengo makubwa ya kuhakikisha sehemu ya mapato kwenye Pato la Taifa (revenue to GDP ratio) inafikia zaidi ya asilimia 14.1, kutoka kiwango cha asilimia 13.7 mwaka 2024/25,” alisema Mwenda.


Alibainisha kuwa mikakati ya Menejimenti, ikiwemo kuanza kwa Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS), itasaidia kuimarisha uwazi, ufanisi, na mshikamano wa kuaminiana kati ya TRA na walipakodi.


Kamishna Mwenda alisisitiza kuwa utekelezaji wa mikakati hiyo ni muhimu ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanaendelea kuimarisha miradi ya maendeleo, kukuza uchumi, na kuhakikisha kila mlipakodi anaona thamani ya kodi anayolipa.




Ends...

Post a Comment

0 Comments