ABOOD NA TILISHO HATARINI KUSITISHIWA VIBALI VYA OFISI ARUSHA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Hatua hiyo imekuja baada ya TARURA kubaini kuwa wamiliki wa ofisi hizo wamekuwa wakizigeuza ofisi zao kuwa vituo rasmi vya mabasi, hali inayosababisha msongamano mkubwa wa magari, usumbufu kwa watumiaji wa barabara na kuhatarisha usalama wa barabara katika maeneo hayo.
Akizungumza leo Januari 2,2016 na waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha, Mhandisi Nicolas Francis, amesema ofisi yake imewaandikia barua za onyo mara kadhaa, lakini wamiliki hao wameendelea kukaidi maelekezo ya mamlaka hiyo.
“Tulitoa vibali kwa sharti la kutotumia hifadhi ya barabara kwa maegesho ya magari au mabasi. Hata hivyo, wamekuwa wakikiuka masharti hayo kwa makusudi, jambo linalolazimisha TARURA kuchukua hatua kali za kisheria,” amesema.
Ameeleza kuwa uwepo wa mabasi katika ofisi hizo unasababisha msongamano mkubwa kwenye barabara kuu ya Arusha–Namanga pamoja na barabara ya kutoka Mianzini Mataa hadi Stendi Kuu ya Mabasi Arusha, hali inayosababisha ucheleweshaji wa safari na hatari kwa watumiaji wa barabara.
Mhandisi Francis ameongeza kuwa mmiliki wa mabasi ya TILISHO hana kibali chochote cha kuendesha maegesho ya mabasi katika ofisi yake iliyopo eneo hilo, lakini bado anaendelea kufanya shughuli hizo kinyume cha sheria.
“BM, ABOOD na TILISHO hawana vibali vya maegesho katika ofisi zao. Endapo hawataacha mara moja, tutawatoza faini nzito na kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kusitisha vibali vyao,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa TARURA, baadhi ya wamiliki wa ofisi hizo walidai kupewa ruhusa ya kuweka paving katika maeneo yao ya biashara, wakidai waliunga mkono agizo la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, la kupendezesha maeneo ya biashara. Hata hivyo, TARURA imeeleza kuwa ruhusa hiyo haikuwahi kuruhusu matumizi ya hifadhi ya barabara kama maegesho ya mabasi.
Hatua hiyo imekuja kufuatia wananchi wa Jiji la Arusha kuendelea kulalamikia vitendo vya baadhi ya mamlaka kutoa vibali bila usimamizi madhubuti, wakisema matumizi holela ya maeneo yasiyoruhusiwa kwa maegesho ya mabasi yamekuwa chanzo kikuu cha msongamano mkubwa wa magari, usumbufu kwa watembea kwa miguu na ajali za mara kwa mara ndani ya jiji.
TARURA imesisitiza kuwa haitavumilia tena ukiukwaji wa sheria za matumizi ya barabara, na imewataka wamiliki wote wa ofisi za mabasi kuhakikisha wanazingatia masharti ya vibali walivyopewa kwa maslahi ya usalama wa barabara na ustawi wa Jiji la Arusha.
Ends..


0 Comments