MGOGORO MZITO WAFUKUTA CHAMA CHA AAFP ,MWENYEKITI TAIFA AMLIMA BARUA NZITO KWA MSAJILI KATIBU WAKE ,VIONGOZI WA MIKOA WATOA TAMKO ZITO HAWANA IMANI NA KATIBU TAIFA.

Mgogoro Mkali Katika Chama cha Siasa cha AAFP: Viongozi wa Mikoa Waibua Tu­huma Dhidi ya Uongozi wa Taifa

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


ARUSHA, Januari 5, 2025 – Chama cha Siasa cha AAFP kimeingia katika mgogoro mkubwa wa uongozi baada ya viongozi wa mikoa kuibua tuhuma dhidi ya viongozi wa ngazi ya taifa, ikiwemo Mwenyekiti na Katibu Mkuu, kwa kuendesha chama kwa maslahi yao binafsi bila kushirikisha viongozi wa mikoa na kutofanya mikutano mikuu kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha, Mwenyekiti wa AAFP Mkoa wa Arusha, Mgina Mustafa, na Mwenyekiti wa AAFP Mkoa wa Kilimanjaro, Flora Samuel Luka, walisema hawana imani na uongozi wa taifa, na kwamba baadhi ya mikutano ya chama inafanyika kinyume na taratibu rasmi. Walisema mikutano hiyo inajumuisha wajumbe wa kinyume ili kuhalalisha maamuzi yasiyo sahihi.


Mwenyekiti wa AAFP Kilimanjaro, Flora Luka, aliitaka Kamati Kuu ya chama kuhakikisha inaitisha vikao halali vya kisheria, kwa mujibu wa katiba ya chama. Flora alisema uhalali wa maamuzi ya chama hauwezi kujengwa juu ya taratibu zisizo rasmi ambazo hazijashirikisha wajumbe halali kutoka mikoa yote.

“Uhalali wa vikao vya Halmashauri Kuu au Mkutano Mkuu hauwezi kupitishwa bila ushiriki wa wajumbe halali kutoka kila mkoa. Kauli hii inapaswa kutafsiriwa kwa vitendo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima,” alisema Flora.

Aliongeza kuwa, kwa zaidi ya miaka sita ndani ya AAFP, hajawahi kushiriki kikao chochote cha Halmashauri Kuu au Mkutano Mkuu, licha ya kuwa mjumbe halali. Pia alibainisha kuwa katiba ya sasa ya chama ilipitishwa bila ushiriki wa wajumbe wa mikoa, jambo linalotia mashaka juu ya uhalali wa maamuzi na kuhatarisha uaminifu wa wanachama.

Flora Luka Mw/kiti AAFP K/NJARO

 Flora, ambaye pia ni mgombea wa ubunge Jimbo la Moshi Mjini kupitia AAFP, aliitaka Kamati Kuu kuitisha kikao halali cha Halmashauri Kuu kabla ya Januari 30, kikiwa na wajumbe halali kutoka kila mkoa, ili kurejesha imani ya wanachama, kuimarisha mshikamano, na kulinda mustakabali wa chama.

Naye Mwenyekiti wa AAFP Mkoa wa Arusha, Mgina Mustafa, amemtuhumu Katibu Mkuu wa Taifa, Rashird Ray, kwa kukiuka katiba na kuvuruga misingi ya uongozi wa chama. Mustafa alisema Katibu Mkuu amekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Mwenyekiti wa chama na kuibua mgogoro mkubwa wa kiuongozi.

“Kwa makusudi au kwa uzembe, Katibu Mkuu amemnyima Mwenyekiti wetu, Sudi Said Sudi, haki ya kikatiba ya kuitisha kikao cha halmashauri. Huu ndiyo mzizi wa mgogoro wa kwanza ndani ya chama,” alisema Mustafa.

Mgogoro wa pili, aliendelea, unatokana na kauli ya Katibu Mkuu Taifa wakati wa salamu za Mwaka Mpya, ambapo alidai kuwa hawajibiki kwa viongozi wakuu wa mikoa. Kauli hiyo, Mustafa alisema, ni ya kudhalilisha na inaashiria dharau ya makusudi au kutokujua muundo na majukumu ya uongozi wa chama.

Mustafa alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ni viongozi wakuu wa chama, wakiwemo wenyeviti na makatibu wa ngazi mbalimbali, idadi inayokidhi masharti ya kikatiba ya koramu na hivyo kuwa na mamlaka kamili ya kufanya maamuzi ya chama. Aliongeza kuwa Katibu Mkuu Taifa aliikiri wazi kuwa endapo Halmashauri Kuu itakutana na kuamua kumbadilisha Katibu Mkuu, uamuzi huo utakuwa halali.

Kutokana na hali hiyo, Mgina Mustafa amemtaka Katibu Mkuu Taifa kurejea hadharani, atengue kauli yake, na aeleze wazi kuwa anawatambua na kuwajibika kwa viongozi wakuu waliopo mikoani, kwa mujibu wa katiba ya AAFP.

 Alisisitiza kuwa lengo la uongozi wa AAFP Arusha si kuvuruga chama, bali kulinda mshikamano, katiba, na demokrasia ya ndani ya chama. Hata hivyo, alionya kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, mgogoro huo utaendelea kudhoofisha mustakabali wa chama.

Viongozi hao pia wameshtusha kwa kutishia kumwandikia barua Msajiri wa Vyama vya Siasa ili kuwalazimisha viongozi wa Taifa kurekebisha mwenendo wa kidikteta na kuanza kushirikisha viongozi wakuu wa mikoa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa AAFP Taifa, Sudi Said Sudi, amethibitisha kuwepo kwa mgogoro mkubwa na Katibu Mkuu Rashird Ray, akisisitiza kuwa matatizo hayo yametokana na taratibu za katibu kutekeleza shughuli za chama bila kushirikisha uongozi wa taifa.

“Ninaungana na kauli ya viongozi wa mikoa kuwa kweli nina mgogoro na Katibu wangu Rashird Ray, ambaye amekuwa akifanya taratibu bila kunishirikisha. Zaidi ya hayo, amekuwa akikusanya wajumbe kutoka mitaani na kufanya mikutano, akijihakikishia kuhalalisha mambo ya chama kwa maslahi yake binafsi,” alisema Sudi.

Sudi alifafanua kuwa mgogoro huo umeibuka rasmi hadharani ndani ya kipindi cha miezi sita, na kumshangaza kuona mikutano ikifanyika ikileta wajumbe kutoka mitaani bila idhini ya uongozi wa juu wa chama. Alisisitiza kuwa hali hii imesababisha viongozi wa mikoa kutoa tamko lao kuwa Katibu Mkuu ndiye kikwazo kikuu katika uendeshaji wa chama.

Naye Katibu Mkuu wa Taifa, Rashird Ray,alipohojiwa alisema haoni kama kuna mgogoro ndani ya chama ila alikiri mwenyekiti wake kuandika barua kwa msajili wa vyama juu ya fukuto ndani ya chama hicho na wameshaitwa kujadili changamoto hizo.

Alibainisha kuwa mikutano imetokea kila baada ya miaka mitano kwa mujibu wa katiba yao , alisisitiza kuwa hayupo mtu wa kutaka mkutano ufanyike muda wowote anapotaka . Alisema mara ya mwisho mkutano ulifanyika mwaka 2023 na itafanyika tena mwaka 2028. 

Alisisitiza kuwa hana mgogoro na Mwenyekiti wake na kwamba Mwenyekiti wa mkoa wa Kilimanjaro, Mgina Mustafa, amekuwa akihudhuria mikutano hiyo, hivyo si kweli kama huwa hashirikishwi 

Mwisho


Post a Comment

0 Comments