MEYA IRANGHE ATOA KARIPIO KALI KWA MAMLAKA ZA USAFI ARUSHA, ATANGAZA MPANGO MKAKATI WA USAFI 2026

 By Joseph Ngilisho – ARUSHA

MEYA IRANGHE ATOA KARIPIO KALI KWA MAMLAKA ZA USAFI ARUSHA, ATANGAZA MPANGO MKAKATI WA USAFI 2026


MASTAHIKI Meya wa Jiji la Arusha,  Maximilian Iranghe, ametoa karipio kali kwa mamlaka zote zinazosimamia usafi wa mazingira jijini humo, akizitaka kusimamia kwa ukamilifu na kwa kiwango cha juu suala la usafi ili kukomesha tatizo la uchafu uliokithiri katika kata, mitaa, maeneo ya wazi na masoko ya jiji hilo.

Meya Iranghe amesisitiza kuwa hali ya uchafu haiendani kabisa na hadhi ya Jiji la Arusha, ambalo ni kitovu kikuu cha utalii wa kimataifa, biashara na mikutano.

“Jiji la Arusha ni jiji la kitalii, ni aibu kubwa kuwa na mazingira machafu,” alisema kwa msisitizo.

Uzinduzi wa Mpango wa Usafi 2026

Kauli hiyo ameitoa leo Januari 02, 2025, wakati akizindua rasmi Mpango wa Usafi wa Mazingira kwa Mwaka 2026, ambao utatekelezwa kila siku ya Jumamosi ya kila wiki jijini Arusha.

Katika hotuba yake, Meya alibainisha kuwa usafi si wa siku moja bali ni jukumu la kila siku na la kila mwananchi, akisisitiza kuwa kila mtu anatakiwa kushiriki kikamilifu katika eneo lake la kazi na makazi.Uzinduzi huo umefanyika katika kata ya Sokon one na ulienda sanjari na kushiriki usafi kwa kutoa taka kwenye mitaro na kufagia katika eneo la soko, Dampo.

Iranghe aliwataka Afisa Afya wa Jiji la Arusha pamoja na Maafisa Afya wa Kata kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria za usafi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu au taasisi zitakazobainika kuchafua mazingira.

Aidha, aliagiza viongozi hao kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki mara kwa mara katika shughuli za usafi ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama, safi na rafiki kwa afya ya binadamu.

Maboresho ya Miundombinu

Akizungumza kuhusu changamoto ya maji na barabara, Meya alisema Jiji la Arusha limejipanga kuboresha miundombinu ya barabara na mitaro, hususan kipindi hiki cha mvua za masika, ili kuhakikisha maji yanapita kwa urahisi na barabara zinapitika wakati wote.

“Tumedhamiria kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya miundombinu; tunachoomba ni ushirikiano wa wananchi,” aliongeza.

Kauli ya Diwani wa Kata ya Sinon

Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika katika Kata ya Sokon One, ikihudhuriwa na madiwani, watendaji wa kata na mitaa pamoja na wananchi.

Diwani wa Kata ya Sinon,  Peter Inyasi, alisema kuwa madiwani kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa wamejipanga kusimamia kikamilifu zoezi la usafi katika maeneo yao ili kuhakikisha uchafu unadhibitiwa mapema kabla haujaleta madhara.

Aliwataka wananchi kuacha kutiririsha maji machafu kwenye makazi ya watu na kushiriki kikamilifu kufanya usafi kila siku, akibainisha kuwa kata za pembezoni mwa jiji ndizo zimeathirika zaidi na uchafu, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na miundombinu mibovu.

Uzinduzi wa mpango huo unaashiria dhamira ya dhati ya uongozi wa Jiji la Arusha katika kulinda afya ya wananchi, mazingira na taswira ya jiji la kitalii, huku ushirikiano wa wananchi ukitajwa kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya mpango huo.








Post a Comment

0 Comments