WAUMINI WANNE WAFA KANISANI KWA KUANGUKIWA NA UKUTA WAKISALI DODOMA!

UKUTA WA KANISA WAPOROMOKA DODOMA, WATU WAWILI WAFARIKI PAPO HAPO, WENGINE 18 WAJERUHIWA

Na ArushaDigital – Dodoma


Watu wanne wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa Kanisa la Anglikana wakati wa ibada ya ubatizo iliyofanyika Desemba 23, 2025 katika Parishi ya Wiliko, Dinari ya Mpwayungu, wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika, Dkt. Dickson Chilongani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa miongoni mwa waliofariki dunia ni mke wa Kasisi wa Dinari ya Mpunguzi, Dina Machela.

Akizungumza jana kuhusu tukio hilo la kusikitisha, Dkt. Chilongani amesema kuwa siku ya tukio kulikuwa na ibada ya ubatizo kanisani hapo, ambapo kabla ya ibada kukamilika kulionekana dalili za mvua kunyesha.

Amesema kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, mchungaji aliyekuwa anaongoza ibada aliamua kuhitimisha mapema ili kuwawezesha waumini kutawanyika na kurejea majumbani mwao kwa usalama.

“Baadhi ya waumini walifanikiwa kuondoka mara moja, lakini wengine waliamua kubaki ndani ya kanisa na pembezoni mwa ukuta wakijikinga dhidi ya mvua,” amesema Askofu Chilongani.

Ameongeza kuwa mvua ilipoanza kunyesha iliambatana na upepo mkali, hali iliyosababisha mmoja wa kuta za kanisa hilo kuporomoka ghafla na kuwaangukia waumini waliokuwa wamejisitiri karibu na eneo hilo.

“Katika tukio hilo, watu wawili walifariki dunia papo hapo, huku wengine 18 wakipata majeraha ya viwango mbalimbali,” amesema.

Aidha, amesema watu wengine wawili, akiwamo mke wa Kasisi wa Dinari ya Mpunguzi, walifariki dunia wakiwa njiani wakikimbizwa katika vituo vya afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Askofu Chilongani ameeleza masikitiko makubwa ya kanisa kufuatia tukio hilo na kutoa pole kwa familia za marehemu pamoja na waumini walioathirika, huku akisisitiza umuhimu wa tahadhari zaidi katika majengo ya ibada, hasa nyakati za hali mbaya ya hewaNB 

NB :picha haihusiani na STORY 

Ends

Post a Comment

0 Comments