UCHUNGUZI WA KINA WAANZA AJALI YA HELIKOPTA KILIMANJARO, WATAALAMU TCAA NA AAI WAWEKA KAMBI BARAFU
Na Arushadigital, Moshi – Kilimanjaro
Wataalamu kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kushirikiana na Kitengo Maalumu cha Uchunguzi wa Ajali za Ndege (AAI) wameweka kambi katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, eneo la Barafu, kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo na mazingira ya ajali ya helikopta ya kampuni ya uokoaji Kilimedair, ajali iliyosababisha vifo vya watu watano.
Akizungumza leo Desemba 25, 2025 mjini Moshi, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Kuji, amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika, huku akibainisha kuwa timu za uchunguzi zimefika eneo la tukio na zinaendelea na kazi ya kitaalamu kwa kuzingatia taratibu zote za kimataifa za uchunguzi wa ajali za anga.
“Hadi sasa hatuwezi kutoa hitimisho lolote. TCAA na AAI wako eneo la tukio, wanakusanya vielelezo, taarifa za kiufundi na ushahidi mwingine muhimu ili kubaini chanzo halisi cha ajali na mazingira yaliyoisababisha,” amesema Kamishna Kuji.
Kwa mujibu wa TANAPA, waliofariki dunia katika ajali hiyo wametambuliwa kuwa ni David Plos (30) na Anna Plosova (30), watalii na raia wa Jamhuri ya Czech. Wengine ni Costantin Mazonde (42), raia wa Zimbabwe ambaye alikuwa rubani wa helikopta hiyo na mkazi wa Soweto, Moshi; Jimmy Daniel (32), daktari wa kampuni ya uokoaji ya Kilimedair na mkazi wa Rau, Moshi; pamoja na Inocent Mbaga, muongoza watalii (Guide) aliyekuwa katika safari hiyo.
Kamishna Kuji amesema watalii hao walianza safari yao ya kupanda Mlima Kilimanjaro tarehe Desemba 20, 2025, wakitumia njia ya Machame, chini ya Kampuni ya Utalii ya Mikaya Tours, katika mpango wa safari ya siku sita. Inadaiwa helikopta hiyo ilikuwa ikitoa huduma za uokoaji wakati ilipopata ajali katika eneo la Barafu, mojawapo ya maeneo yenye changamoto kubwa za hali ya hewa na miinuko mikali juu ya mlima huo.
TANAPA imeeleza kuwa ajali hiyo ilihusisha helikopta ya Kampuni ya Kilimedair aina ya Airbus, huku uchunguzi ukiendelea kubaini masuala ya kiufundi, hali ya hewa, mawasiliano, pamoja na rekodi nyingine muhimu kabla ya ajali kutokea.
Katika hatua nyingine, TANAPA imewahakikishia Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuwa usalama wa watalii na shughuli za utalii katika Mlima Kilimanjaro unaendelea kupewa kipaumbele, na kwamba taarifa kamili ya uchunguzi itatolewa mara tu kazi hiyo itakapokamilika na mamlaka husika.
Ajali hiyo imeacha msiba mkubwa kwa familia za marehemu, sekta ya utalii na anga nchini, huku uchunguzi huu ukitarajiwa kutoa mwanga juu ya tukio hilo na kusaidia kuimarisha zaidi mifumo ya usalama wa anga na uokoaji katika maeneo ya milima na hifadhi za taifa.
Ends.

0 Comments