MKE WA MCHUNGAJI AJITUNDIKA NA KUJINYONGA HADI KUFA CHUMBANI,ALIKOPA MAMILIONI YA FEDHA ZA KANISA

MWANAMKE AFARIKI KWA KUJINYONGA NKASI, RUKWA

By Arushadigtal-RUKWA

RPC RUKWA-SHADRACK MASIJA

Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Joyce Baton Mwasumbi, mkazi wa Kijiji cha Kanazi, wilayani Nkasi mkoani Rukwa, amefariki dunia baada ya kujinyonga ndani ya chumba chake kwa kutumia kanga.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanazi, Rudis Ulaya, amesema tukio hilo limetokea leo Jumatano, Desemba 24, 2025, majira ya saa 2:00 asubuhi. Amesema marehemu ambaye alikuwa mke wa Mchungaji wa Kanisa la EAGT katika kijiji hicho, alijinyonga wakati mume wake akiwa kanisani akifanya shughuli za upaliliaji pembezoni mwa jengo la kanisa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mume wa marehemu, Mchungaji Ibrahimu Mwaipopo, aliingia chumbani muda mfupi baada ya kurejea kutoka kanisani na kumkuta mkewe akiwa amejitundika na bado akionekana kuwa hai. 


Alidaiwa kuchukua kisu na kukata kanga aliyojitundikia kwa lengo la kuokoa uhai wake, hata hivyo juhudi hizo hazikufanikiwa kwani marehemu alipoteza maisha muda mfupi baadaye.

Mwenyekiti Ulaya ameeleza kuwa katika mahojiano aliyoyafanya na mume wa marehemu, alieleza kuwa huenda chanzo cha tukio hilo kikahusishwa na msongo wa mawazo uliotokana na deni, ambapo marehemu alidaiwa kukopa fedha za kanisa hilo. 


Ameongeza kuwa katika siku za hivi karibuni marehemu alionekana kuwa na huzuni na kukosa furaha kutokana na deni hilo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo kabla ya kuchukua hatua zaidi za kisheria.

Aidha, Kamanda Masija ameitaka jamii kuendeleza utamaduni wa kushirikishana changamoto wanapokumbwa na matatizo ya kimaisha badala ya kuchukua maamuzi magumu na hatarishi kama kujitoa uhai.


Post a Comment

0 Comments